USANIFU MAJENGO NA UJENZI – 27 KULIPULIWA KWA JENGO

KITABU: FOUNTAINHEAD.

AUTHOR: AYN RAND.

1. Howard Roark anaenda kwa Dominique na kumwambia anataka amsaidie jambo. Dominique anakubali. Anamwambia usiku wa saa tano aende na gari yake karibu na mradi wa Cortlandt na kujifanya anahitaji msaada kutoka kwa mlinzi wa eneo. Kisha watasogea umbali kama wa kilomita moja na eneo hilo la ujenzi na Dominique atashuka na kulala chini.

2. Usiku wa siku hiyo Dominique anaondoka na kupitia kwenye nyumba ya marafiki wa familia kisha anaenda eneo la tukio na kufanya kama alivyoagizwa na Howard Roark.

3. Howard Roark anafika baada ya Dominique kumuondoa mlinzi na kulipua majengo hayo ya mradi wa Cortlandt kwa mabomu. Inatokea milipuko mikubwa inayoharibu kabisa majengo hayo.

4. Dominique anasahau kulala chini kama alivyoagizwa na Howard Roark, hivyo milipuko inamfikia na kumjeruhi. Japo anaonekana ni mwenye furaha na hajali kuhusu majeraha hayo lakini anavuja damu nyingi mpaka anapoteza fahamu.

5. Dominique anakuja kupata fahamu na kujikuta yuko chini ya uangalizi na pembeni yake yupo mume wake Gail Wynand. Anajikuta ana majeraha na alikaa hospitali kwa muda mrefu bila kujijua.

6. Howard Roark anakamatwa na polisi na kupelekwa mahabusu. Gail Wynand anafika na kumwekea dhamana, hivyo anatoka nje kwa dhamana wakati uchunguzi wa kesi yake ukiendelea.

7. Howard Roark anafika kutembelea Dominique ambaye bado ni mgonjwa kitandani na wanaongea kwa kirefu. Howard Roark anamwambia hawezi kujulikana kwa sababu uhusiano wao haujulikani na yeye anafahamika kama mke wa Gail Wynand. Dominique hajali sana juu ya kujulikana.

8. Gordon L. Prescott na Gus Webb wanasema hawajui sababu iliyopelekea Howard Roark kutaka kulipua mradi wa ujenzi wa Cortlandt.

9. Peter Keating yuko nyumbani kwake hataki kuhusishwa sana na tukio hilo bali anasisitiza kwamba Howard Roark hana hatia. Peter Keating anaandika ujumbe kwamba wamwache Howard Roark, anasisitiza kwamba waachane na Howard Roark kwani milipuko ni kitu cha kawaida.

10. Magazeti ya Gail Wynand yanaandika makala nyingi za kumtetea Howard Roark. Lancelot Clokey ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa magazeti ya Gail Wynand kwa kudai kwamba hayana maadili anaandika kwamba Howard Roark anathibitisha kuwa mtu mwovu kwa sababu anatetewa na watu waovu.

11. Kesi ya Howard Roark inajadiliwa kila mahali na vyombo mbalimbali vya habari.

12. Kampeni za kugomea kusoma Magazeti ya Gail Wynand zinaendelea kila mahali. Baadhi ya makampuni yanakataa kuendelea kufanya nao kazi kwa sababu ya kampeni hizo.

13. Gail Wynand anamwonya Ellsworth Toohey kukaa kimya kabisa juu ya suala zima la kesi ya Howard Roark. Anataka magazeti hayo yafanye kazi ya kumtetea Howard Roark mpaka mwishoni aweze kushinda kesi hiyo kwa msukumo wa mtazamo wa watu dhidi ya mahakimu.

14. Peter Keating hataki kuzungumza na waandishi wa habari na ameamua kubaki nyumbani haendi kazi wala popote. Anasisitiza kwamba watu na hususan wanahabari wamwache wasijaribu kumsumbua.

15. Mama yake Peter Keating anamwita Ellsworth Toohey na kumwomba ajaribu kumzungumza Peter Keating kwani anaonekana hayuko sawa. Hata kutoka nje ya nyumba wala hataki kwenda popote amekaa tu chumbani kwake, hivyo anamkaribisha Ellsworth Toohey chumbani kwa Peter Keating.

16. Peter Keating anafurahi kumwona Ellsworth Toohey na kusema alitamani sana kukutana naye. Ellsworth Toohey anajaribu kutumia nafasi hiyo kumshawishi Peter Keating kumpa siri ya ukweli juu ya ni nani aliyefanya kazi ya Usanifu wa majengo ya mradi wa Cordlandt. Peter Keating anasisitiza kwamba amefanya kazi hiyo mwenyewe na hataki maswali zaidi.

17. Ellsworth Toohey anaendelea kusisitiza kwa kutumia mbinu mbalimbali bila mafanikio. Ellsworth Toohey anamtishia Peter Keating na kuonyesha na Peter Keating kwa sababu ya kupaniki anatoa ile karatasi ya mkataba walioandikia na Howard Roark kwenye droo na kumkabidhi Ellsworth Toohey.

18. Ellsworth Toohey anafurahi sana na kumsifia sana Peter Keating kwa kumpa nyaraka hiyo. Ellsworth Toohey anamwambia Peter Keating kwamba kupitia nyaraka hiyo atapata kila kitu na atahakikisha anamsaidia ili kila kitu kiende kwa faida yake.

19. Ellsworth Toohey anamsimulia Peter Keating kwa kirefu sana nia na malengo ya falsafa anayoipigania. Anamwambia wazi kwamba yeye wala hana nia njema yoyote ya kupigania maadili mema bali anahitaji nguvu za mamlaka kupitia kuwafanya watu ni watumwa wa vitu wanavyoaminishwa kwamba ni maadili.

20. Ellsworth Toohey anafunguka kwa Peter Keating juu ya mpango wake mzima wa mfumo anaotumia kutumikisha watu na mwishoni kuwa na nguvu za kimamlaka kupitia ushawishi baada ya watu wote kuwa dhaifu.

21. Ellsworth Toohey anafanya hivyo kwa kuhubiri kwamba unyonge ni utakatifu na watu wanapaswa kuwa sawa na kutojithamini kama wanavyothamini wengine. Ellsworth Toohey anasema pia watu wanapaswa kutojali furaha zao wala kujiamini na kwa namna hiyo atawageuza wote ni watu. Peter Keating anapigwa na butwaa na kumshangaa Ellsworth Toohey. Ellsworth Toohey anamwambia Peter Keating, je anafikiri Howard Roark ni mtu atakayeweza kukubaliana nao? Peter Keating anajibu hapana, hivyo anamwambia basi aache kumshangaa na asimfikirie kwamba yeye ni mtu mwema sana bali waungane kukamata nguvu za kimamlaka kupitia ushawishi huo.

22. Magazeti ya Gail Wynand yanaandika makala inayomzungumzia vibaya Howard Roark bila Gail Wynand kujua. Gail Wynand anakuja kugundua na kukasirika sana.

23. Kutokana na kukiuka maagizo yake Gail Wynand awafukuza kazi wafanyakazi wanne mameneja kwenye kampuni yake akiwemo Ellsworth Toohey.

24. Unatokea mgomo mkubwa wa wafanyakazi wa “The Banner” dhidi ya Gail Wynand ambao wana madai kwamba wafanyakazi waliofukuzwa warudishwe kazini na pia kesi dhidi ya Howard Roark iandikwe kwa uhuru na kufuata maadili ya uandishi.

25. Gail Wynand anaingia ofisini na kufanya kazi nyingi mwenyewe akisaidiana na baadhi ya wafanyakazi watiifu kwake akiwemo Alvah Scarret.

26. Gail Wynand anajaribu kuajiri wafanyakazi wengi wapya, wengine hawana uwezo mkubwa na wengine anaishia kuwafukuza katika kuziba nafasi zilizoachwa wazi na wafanyakazi walioingia kwenye mgomo.

27. Dominique anamfuata Howard Roark kumsaidia majukumu ya ofisini na wanafanya kazi sana mpaka kulala huko huko. Dominique anaonekana kufanya kazi zaidi na mwenye nguvu zaidi.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *