NANI ANAKUSHAURI KUHUSU UJENZI?
Wakati mwingine mradi wa ujenzi unaweza kuharibika sio kwa sababu ya ufundi duni au usimamizi usiofaa bali kwa sababu kuchukua ushauri kwa kila mtu bila kupima umetokea wapi. Kwa sababu pengine ya mazoea au ukaribu uliopo baina ya watu, baadhi ya watu wamekuwa wakichukua ushauri kuhusu ujenzi kutoka kwa watu wa kawaida wasiojua chochote kuhusu ujenzi na kuutekeleza. Ushauri huu umekuwa ukisababisha sio tu kuharibika kwa ujenzi bali hata kuharibika kwa mahusiano baina ya wataalamu wanaojenga na mmiliki wa jengo.
Mara nyingi watu wa karibu wasiokuwa na uzoefu wowote na ambao hawana taarifa zilizoko kwenye wakati wamekuwa wakiwaaminisha wamiliki kwamba mradi aidha unakosewa au kuna ubadhirifu unafanyika, na kwa sababu mmiliki anaambiwa hivyo na mtu wa karibu basi anamwamini na kuchukua hatua. Mara nyingi mmiliki huja kugundua kwamba alifanya makosa akiwa ameshachelewa sanana hivyo kujutia kwa nini hakuwa makini kujiridhisha kama yule anayemshauri ni mtaalamu kweli anayejua anachoshauri au anafanya tu hivyo ili kutaka kumfurahisha.
Ikiwa unataka kazi ya ujenzi ifanyike kwa usahihi ni muhimu kufuata utaratibu ambao tumekuwa tunashauri hapa mara kwa mara katika kufanikisha ujenzi wako badala ya kusikiliza na kuzingatia kila mtu. Ziko taratibu nzuri sana ambazo zikifuatwa basi kazi yako itafanyika vizuri na kwa usahihi na kwa gharama sahihi pia bila kutegemea kuchukua ushauri usio sahihi kutoka kila mahali. Hakuna kitu kinachoharibu kazi za kitalaamu kama kuchukua ushauri usio sahihi au kutochukua ushauri kabisa. Hivyo ni muhimu sana kuwa makini sana juu ya ni wapi unapochukua ushauri na kufanya maamuzi juu ya mradi wako wa ujenzi.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255 754 584 270.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!