KUFANYA MAAMUZI SAHIHI KWENYE UJENZI DHIBITI HISIA ZAKO.

Kuna baadhi ya maeneo kwenye ujenzi yanayohitajika kufanya maamuzi sahihi zaidi kuliko maeneo mengine. Lakini kwa sababu ya udhaifu mkubwa tulionao binadamu huwa tunaongozwa na hisia na hivyo kupoteza umakini kwenye kile haswa ambacho tunapaswa kufanya. Hili limepelekea kuishia kufanya maamuzi yasiyo sahihi na kusababisha madhara na hasara kubwa kwetu na hatimaye kuishia kwenye majuto katika mambo ambayo endapo tungefanya kwa usahihi tusingejutia.

Eneo la kwanza na muhimu sana kwenye ujenzi kabla ya hatua yoyote ni kuhakikisha unapata mtaalamu mwenye uwezo na uzoefu kwa ajili ya kukufanyia kazi ya ushauri wa kitaalamu sambamba na michoro sahihi ya ramani ya ujenzi wa mradi wako. Hata hivyo eneo hili licha ya umuhimu mkubwa wa kufanya maamuzi haya sahihi watu wengi kwa kuongozwa na hisia wamekuwa wakikwepa wataalamu kwa kuogopa aidha gharama au hofu nyingine yoyote isiyo na mashiko. Hili limepelekea aidha wao kuishia kutumia gharama kubwa kujenga jengo la hovyo au kujenga jengo la chini ya kiwango kwa kutokutumia mtaalamu mwenye uwezo na uzoefu.

Suala la gharama kwa hatua hii sio kubwa ukilinganisha na hasara na majuto ambayo mtu anakwenda kutumia katika kununua vifaa vya ujenzi vya mamilioni na kuishia kuvijenga katika jengo duni au ambalo halijazingatia ubora na utaalamu. Sasa mwishoni mtu anapokuja kugundua kwamba gharama zile hazikuwa kubwa ukilinganisha na matatizo yaliyojitokeza baada ambayo ni makosa ya kitaalamu au mwonekano usiovutia wa jengo litakaloishi kwa kipindi pengine cha nusu karne, karne nzima au zaidi ya karne nzima ndipo anajikuta anajuta kwani hawezi tena kubadili na ameshatumia mamilioni au mabilioni ya pesa eneo hilo. Hayo anakuwa aliyafanya kwa kuongozwa na hisia ya hofu kwamba utaalamu ni gharama kumbe anakwenda kutumia gharama kubwa sana kwenye vitu vingine ambavyo vingeweza hata kupungua gharama kupitia ushauri wa kitaalamu.

Eneo jingine muhimu la kuzingatia ili kufanya maamuzi yaliyo sahihi ni eneo la ufundi katika ujenzi. Hili ni eneo jingine ambalo watu hufanya maamuzi kwa kutumia hisia na kutokuhusisha utaalamu vya kutosha kwa kuogopa gharama na hivyo kufanyika makosa mengi yenye gharama kubwa kuliko ile gharama iliyokuwa inadhaniwa kuokolewa. Katika hali ya kawaida fedha hutafutwa na kupatikana lakini kuna makosa yakishafanyika ambayo hayakuhitaji fedha nyingi kuyakabili basi yanaleta madhara makubwa ambayo mtu yanakuja na gharama kubwa kwa kipindi chote cha matumizi ya jengo au yatahitaji tena kukuingiza hasara nyingine kuyatatua.

Sasa, kinachopaswa kufanyika ni nini? Kinachotakiwa kufanyika ni mtu kudhibiti hisia zako na kuweka kipaumbele kwenye ubora kwanza kabla hujaanza kuogopa gharama ambazo nazo mara nyingi sio kubwa katika uhalisia bali tu ni mtu anaongozwa na hofu ya kwamba gharama ni kubwa. Hili binafsi nimeweza kuliona katika uhalisia pale ambapo nimekutana na wateja ambao wameogopa kutumia wataalamu wenye viwango vya juu katika taaluma kama vile wahandisi na wasanifu katika ujenzi na badala yake kutumia wataalamu wenye viwango vya chini zaidi lakini ukichunguza gharama zao zinalingana au kukaribia kulingana. Hivyo kilichomuongoza mtu kufanya yale maamuzi sio ukubwa wa gharama bali ile hofu kwamba gharama ni kubwa tofauti na ilivyo katika uhalisia.

Hivyo basi ikiwa mtu utaacha kuongozwa na hisia pale unapofanya maamuzi katika miradi ya ujenzi ambayo inahusisha maamuzi yanayohusu fedha nyingi na badala yake kupima faida na hasara kwa kutumia akili na namba na haswa kwa kuangalia madhara ya baadaye, basi unaweza kujikuta unaepuka majuto mengi na makubwa mbeleni. Fanya maamuzi sahihi yatakayokufanya ujivunie baadaye badala ya kujutia.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *