HII NI CHANGAMOTO KATIKA UJENZI.

Moja kati ya tamaduni ambazo tumekuzwa nazo lakini zinatugharimu sana hapa nchini ni pamoja na suala zima la ukweli na uwazi. Kwa miaka ya nyuma kwenye taasisi nyingi hususan za umma suala la uwazi wa taarifa na takwimu nyingine ndani ya taasisi hizo sio jambo lililokuwa linapewa kipaumbele. Inawezekana ni sababu za kisiasa au nyinginezo lakini hata sasa kwa sababu ya kurithi utamaduni huu suala la uwazo sio jambo lilifanikiwa kwa asilimia mia moja.

Utamaduni huu wa kuogopa kuweka taarifa na takwimu wazi kumepelekea watu kufanya maamuzi kwa kuubahatisha kitu ambacho kimepelekea matokeo yasiyo ya kuridhisha sana. Sasa katika ujenzi hili nalo ni changamoto nyingine inayopelekea matokeo yasiyo bora kabisa. Huwa inakuwa kwamba mnapoanza kujadili mradi wa ujenzi na mteja anashindwa kuwa wazi kwenye bajeti aliyoandaa au anayopanga kuitumia katika mradi husika kwa aidha kutoweka wazi kabisa au kupunguza sana kile kiasi alichopanga kutumia.

Mara nyingi watu hufanya hivyo kwa lengo la kuhofia kwamba akiweka wazi bajeti yake basi mtu mwingine au yule mtaalamu aliyenaye ataona kwamba ana fedha nyingi na hivyo kumdai fedha nyingi katika ujenzi huo na badala yake anaamua kuficha au kupunguza ili aonyeshe kwamba bajeti yake ni ndogo na afanyiwe kazi kwa bei rahisi. Sasa kinachotokea hapo ni anafanyiwa kazi za viwango vya fedha hiyo badala ya kufanyiwa kazi ile ambayo angeipenda au kuitaka kwa sababu mtekelezaji alichukulia kwamba hicho ndio kiwango cha fedha kinachopatikana hivyo mteja anastahili kazi ya kiwango cha chini kinyume na matamanio halisi ya mteja.

Licha ya kwamba ni kweli kwamba msimamizi wa mradi anaweza kudai zaidi au kupunguza bei pale anapojua bajeti ya mteja lakini ikiwa unafuata kanuni sahihi msimamizi hawezi kuongeza wala kupunguza bajeti. Lakini kwa kufahamu bajeti halisi ya mteja au kiwango alichopanga kutumia katika ujenzi huo ni rahisi kumshauri kwa usahihi na kufanikisha kufanya kazi hiyo kwa ubora na ufanisi. Hili sio jambo la kuangalia kwa upande hasi hususan kama unafanya kazi na mtu anayetumia kanuni zisizobadilika badilika. Baadhi ya wageni wamekuwa wakiweka uwazi na hilo limesaidia sana katika kupatiwa ushauri sahihi.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *