UJENZI WA GHOROFA KWA BEI NAFUU.

Wako watu wengi sana kwa sasa wanaotamani sana kujenga nyumba za ghorofa kwani wanaamini nyumba za ghorofa zinapendeza na kuvutia zaidi na zinasaidia katika kuokoa eneo la kiwanja ambalo lingejazwa kwa sehemu kubwa zaidi ikiwa mtu ataweka vyumba vyote katika sakafu moja. Lakini watu hawa wengi wamekuwa wakihofia kujenga nyumba ya ghorofa ya kuishi kwa sababu ya kuhofia gharama za ujenzi kuwa juu sana na hivyo aidha kushindwa kumudu au kufanikiwa kumudu lakini kwa gharama kubwa sana ambayo wanahitaji kuitumia kwenye mambo mengine ambayo ni ya msingi pia.

Ni kweli kwamba nyumba ya ghorofa ikifanyika vizuri inaweza kuwa na muonekano maridadi na unaovutuia zaidi na pia inaweza kuokoa nafasi na hata kuwa na nafasi ya kupata hewa nyingi safi na nyepesi zaidi kwa vile vyumba vya juu ukilinganisha na nyumba ya kawaida isiyo ya ghorofa. Ni kweli pia kwamba nyumba ya ghorofa inaongeza gharama zaidi kwa ukubwa ule ule wa mita za mraba ukilinganisha na nyumba isiyo ghorofa kwa mita hizo hizo za ukubwa wa mraba kwa sababu ya kuwepo kwa ule mfumo wa mihimili inayojenga jengo.

Lakini hata hivyo pamoja na hayo bado gharama ya kujenga ghorofa inaweza kuwa nafuu sana karibu saw ana kujenga nyumba isiyo ya ghorofa ikiwa utafanya hivi. Mara nyingi watu wanapoamua kujenga nyumba ya ghorofa huona kwamba wamepata nafasi ya kuwa na nyumba kubwa ya kuishi kwa hiyo hufanya huongeza idadi kubwa ya vyumba tofauti na pale wanapojenga nyumba ya kawaida isiyo ya ghorofa. Mara nyingi sana hii ndio sababu kwamba ujenzi wa ghorofa huwa na gharama kubwa sana. Lakini ikiwa mtu atajenga ghorofa kwa ukubwa ule ule ambao angejenga endapo angejenga nyumba ya chini basi gharama za kujenga nyumba ya ghorofa zitaongezeka kidogo sana kutoka kwenye gharama za kujenga nyumba ya chini.

Hili linatokana na kwamba sehemu kubwa ya gharama inatokana na ukubwa wa nyumba na jengo kwa ujumla la ghorofa linavyoongezeka. Hivyo ghorofa ya gharama nafuu mara nyingi haitokani na ubanaji wa matumizi au kanuni nyingine yoyote ya ujenzi bali inatokana na namna mtu anahakikisha ukubw amita za mraba zinazojengwa hautofautiana sana na kama angekuwa anajenga nyumba ya chini. Hapo gharama za kujenga ghorofa zitaongezeka lakini sio kwa kiasi kikubwa kinacholeta utofauti mkubwa sana wa bei. Hivyo jambo la kuzingatia zaidi ni namna utakavyoweza kudhibiti hisia za kutamani jengo lenye vyumba vingi juu na chini na badala yake kubaki na idadi ile ile ambayo ungefanya endapo ungejenga nyumba ya chini isiyo ya ghorofa.

Hata hivyo hii ni katika hatua ya ujenzi ambayo ndipo gharama kubwa huenda kwa zaidi ya asilimia 95%, lakini kwa hatua ya michoro ile michoro ya mihimili ambayo isingehitajika ikiwa nyumba ni ya chini itahitajika kwa sababu ndio michoro ya mihimili wa jengo kwa jengo lolote la ghorofa bila kujali ukubwa wake. Gharama hizi huwa sio kubwa hivyo haziongezi gharama sana katika jengo zima kwa ujumla lakini mtu unakuwa umepata ushauri sahihi wa kitaalamu unaohitajika kuweza kusimamisha jengo lako la ghorofa. Hivyo huhitaji kuwa na hofu kubwa ya gharama ikiwa unatamani kujenga ghorofa bali unapaswa kuamua na kisha kuchagua kwa usahihi.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *