MABADILIKO YOYOTE YASIYOMHUSISHA MTAALAMU KATIKA MRADI WA UJENZI YANAHARIBU.

Wiki iliyopita nilienda kutembelea eneo moja la ujenzi wa ghorofa ya mtu Dar es Salaam ambayo nilifanya michoro na kuacha msimamizi wa ujenzi maarufu kama “Site Foreman” akiendelea na kazi ya kusimamisha jengo hilo. Kisha nilirudi tena mwisho wa wiki iliyofuata wakati wanaanza kazi ya kupangilia vyumba kwa ajili ya kuhakikisha hakutokea makosa yoyote katika hatua hiyo kwani huja na madhara makubwa baadaye ambayo sio rahisi kuyarekebisha yakiwa yameshafanyika. Tulifanya kazi pamoja na kutoa ufafanuzi kwenye maeneo yaliyokuwa na utata na mwisho tukafikia makubaaliano katika maeneo yote yenye utata tukiwa pamoja na mteja mwenyewe mwenye mradi.

Kisha niliwasiliana na mteja mwenye mradi baada ya siku tatu tukakubaliana tena tukutane eneo la site siku hiyo, na kwa sababu mimi bado nilikuwa Dar es Salaam nilimwambia ni saw ana mchana wa kama saa saba hivi nilifika katika eneo la ujenzi na kukuta ameshafika akitokea mjini. Pale sasa niliambiwa kwamba jana yake walifanya tena mabadiliko mengine kwenye madirisha katika kuhakikisha vyumba vya chini vinakuwa na usalama wa kutosha. Niliangalia yale mabadiliko ambayo katika hali ya kawaida yanaonekana hayana tatizo na wamepatia na kuona mapungufu makubwa.

Ukweli lengo lao lilikuwa linatumia lakini huku wakiwa wameshaanza kuharibu ubora wa jengo na mwonekano wake bila wao wenyewe kugundua kwa sababu hawazijui wala kuzingatia kanuni za kitaalamu katika kufanya maamuzi hayo. Hivyo sasa ilibidi niingilie pale na kutoa mwongozo wa kwamba kwa sababu wamefanya maamuzi yao hayo inabidi kuna mabadiliko zaidi yafanyike ili kuendana na mabadiliko hayo na sio eneo moja peke yake. Wote tulikubaliana hivyo ili kuhakikisaha ule ubora na mwonekano unaendelea kuvutia kama ilivyokuwa mwanzoni kabla ya mabadiliko.

Hiyo ni kusema kwamba kama sio kufika katika eneo la ujenzi na kuhoji kilichofanyika kisha kutaka mabadiliko zaidi ili kuweza kulinda ile hadhi ya jengo lenyewe badi huenda jengo tayari lingeanza kupoteza umaridadi wake na kuonekana halina thamani kubwa. Jambo hili au mambo kama haya yamekuwa yakitokea wakati wote na katika maeneo yote ya ujenzi ninayoyatembelea. Hivyo ni muhimu sana kila maamuzi yanayofanyika katika eneo la ujenzi yazingatie sana ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mtaalamu mwenye uzoefu badala tu ya kufanya maamuzi kienyeji.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *