KWENYE UJENZI MTAZAMO USIO SAHIHI MARA ZOTE UMEKUWA CHANGAMOTO.

Katika miradi ya ujenzi ambayo tumekuwa tunafanya imenipa funzo moja kubwa sana kwenye maisha ambalo sitegemei kulisahau maisha yangu yote. Funzo hili ni nguvu ya mtazamo ambayo ilitokea kwangu binafsi na kunifanya kushangaa jinsi nguvu hii inaweza kuwa na athari kubwa. Nilikuwa kwa muda kidogo nimeshtakia juu ya mwenendo wa moja kati ya watendaji wa juu wa kazi kazini kwetu ambaye ana nafasi kubwa na msimamizi tegemeo sana kwenye ofisi yetu. Nilianza kupewa malalamiko juu ya mwenendo wake kwa muda na watu wa chini yake lakini sikuchukua hatua mara moja kwa sababu ya kutokuwaamini wale wanaonipa malalamiko hayo kama jinsi ninavyomwamini mhusika mwenyewe.

Hili lilipelekea mhusika kuendelea kufanya makosa bila kuwajibishwa kwa sababu ya mtazamo uliojengeka kwamba mhusika huyo ni mtu mwaminifu, mchapakazi na anayejali na hao wanaoleta ripoti zisizofaa kuhusu yeye inawezekana labda wameshindwa tu kuelewana naye wao wenyewe. Kweli na mhusika mwenyewe mara kadhaa amekuwa akisema kwamba hao watu wa chini yake sio watu wazuri na wanasumbuliwa zaidi na tamaa na kujijali wenyewe ndio maana wanazungumza mabaya kuhusu yeye kiasi kwamba tulifikia mpaka hatua ya kuwasimamisha kazi kwa muda. Hivyo mambo yaliendelea kufanyika hivyo na tabia za mhusika huyo zilipozidi kujidhihirisha ndipo ikawa wazi kwamba alikuwa ana changamoto kubwa alizoweza kuzificha kwa muda.

Matatizo yake yalikuwa ni makubwa na yalifikia sehemu ya kuleta athari kubwa sana ofisini kiasi kwamba ililazimika kumchukulia hatua mara moja ya kumsimamisha kazi kwa muda usiojulikana. Kitu kilichonishangaza binafsi ni kwa nini ilinichukua muda mrefu kumchukulia hatua wakati tayari kulikuwa na dalili na malalamiko ya tabia nyingi za kukosekana kwa uadilifu na uaminifu zilizoripotiwa. Kitu nilichogundua ni mtazamo uliokuwa umejijenga kwako kwamba ni mtu mwaminifu, mwadilifu kama mwenyewe alivyokuwa anajitangaza kuwa ni mtu wa kanisani na maombi pamoja na uchapakazi. Ni mpaka tabia za uzembe na udanganyifu zilipokuwa dhahiri kabisa ndipo mtazamo huo ulibadilika na kugundua kwamba mtu huyo amefanya makosa mengi na kwa muda mrefu kabla ya kugundulika.

Sasa kwenye ujenzi kuna aina nyingine ya mtazamo ambayo sio sahihi na inawapelekea wateja wa ujenzi kufanya maamuzi yasiyo sahihi kwao. Mtazamo huu ni kwamba fundi wa kawaida wa mtaani asiye na elimu ya juu kwenye ujenzi anatoza gharama nafuu kuliko mtaalamu wa uhandisi wa usanifu mwenye elimu kubwa ya chuo kikuu. Mtazamo huu umesababisha wateja wengi kutumia mafundi wa mitaani ambao licha ya kwamba wengi wana uzoefu mkubwa katika ufundi lakini wana udhaifu maeneo mengine, kuwapa kazi zaidi na kuwakwepa wataalamu wenye elimu kubwa zaidi kwa hofu hiyo pekee. Nilichokuja kugundua ni kwamba watu hao wanasumbuliwa na mtazamo usio sahihi pekee lakini kwenye uhalisia mambo hayako hivyo.

Mara kadhaa katika kupeleka zabuni au mapendekezo mengine ya kujenga nimekutana mara zote na mafundi wa mtaani ambao wanatoza gharama sawa au kubwa kuliko gharama za wataalamu wenye ujuzi wa juu kitaaluma na kiusimamizi. Hivyo ni vyema sana ikiwa mteja ana mradi kujiridhisha kwenye uwezo na uaminifu katika kazi badala ya kuogopa mtaalamu kwamba atakuwa na gharama kubwa ukilinganisha na fundi wa kawaida wa mtaani. Sisemi kwamba mteja aweke ubaguzi wa aina yoyote bali najaribu kuhimiza kwamba mteja asimwogopa mhandisi kwamba atakuwa na gharama kubwa kwani hilo mara nyingi kwa kazi za kitaalamu sio kweli, kwani huo ni mtazamo usio sahihi.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *