MFUMO WA UENDESHAJI KWENYE MRADI WA UJENZI UTAEPUSHA MAKOSA MENGI.

Mfumo wa Uendeshaji kwenye mradi wa ujenzi ni nini? Mfumo wa uendeshaji kwenye mradi wa ujenzi ni kuwepo kwa utaratibu fulani wenye hatua zote za utekelezaji wa mradi wa ujenzi unaozingatia mambo yote muhimu, ziada na dharura kwenye kutekeleza mradi wa ujenzi badala ya kufuata maelekezo ya mtu mmoja. Hii sio kumaanisha kwamba mradi husika wa ujenzi hautakuwa na mtu wa kusimamia Hapana, mradi unakuwa na msimamizi kama kawaida kwa sababu bila msimamizi lolote linaweza kutokea lakini uwepo wa msimamizi haubadilishi utaratibu uliowekwa.

Hii ni kumaanisha kwamba mfumo wa utekelezaji wa mradi upo ambao unazingatia kila kitu hivyo msimamizi yeyote anayekabidhiwa jukumu la kusimamia mradi huo ataufuata mfumo kama ulivyo badala ya kujiamulia anavyotaka yeye. Hii inakuwa kwamba mwanzoni wakati mradi unaanza kila hatua ya mradi iliwekwa kwenye maandishi na kila kifaa na ufundi unaotakiwa kutumika unajulikana na kujulikana namna unavyokwenda kufanyika. Hili litepelekea kwamba kusiwe na utofauti mkubwa wa ubora kwa miradi yote inayosimamia kwa kufuata mfumo husika na hivyo kuepuka uharibifu na hasara.

Changamoto za kimfumo zinapojitokeza kinachofanyika ni kwamba zinachukuliwa na kujadiliwa kisha mfumo kufanyiwa marekebisho yanayokwenda kukabiliana na changamoto husika. Utaratibu huu unaondoa sehemu kubwa ya uharibifu unaotokana na usahaulifu au uzembe wa kumtegemea mtu mmoja mtaalamu kusimamia na kufanya maamuzi kwa kichwa chake mwenyewe. Uzuri wa mfumo unaondoa utegemezi wa mtu mmoja na kuhakikisha matokeo mazuri ya mwisho hata ikiwa uwezo wa msimamizi sio mkubwa sana. Hata hivyo mfumo wa utekelezaji ndio utaratibu unaotumika katika maeneo mengi makubwa na ambayo yana unyeti mkubwa sambamba na hatari kubwa katika utekelezaji wa miradi husika.

Maeneo ambayo mifumo inalazimika kutumika ni pamoja na kwenye mahospitali makubwa na hususan huduma nyeti, kwenye majengo makubwa na miradi mkubwa ya ujenzi, kwenye kurusha na kuongoza ndege n.k., Mfumo unasaidia kurahisisha utendaji kazi na kuhakikisha ubora kwani hakuna kitu kinachosahaulika wala kufanyiwa maamuzi dhaifu.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *