KIKAO CHA KWANZA KABLA YA MRADI WA UJENZI KUANZA NI MUHIMU SANA.
Siku za hivi karibuni kuna ujenzi wa nyumba moja kubwa ya kuishi umekuwa unaendelea, sasa mradi huo unasimamiwa na msimamizi wa ujenzi peke yake(foreman) ambaye ndiye anahakikisha utekelezaji unazingatia kila kilichofanyika kwenye michoro. Kazi hiyo ya michoro nimeifanya mwenyewe lakini kwenye usimamizi huwa nafika eneo la ujenzi mara chache hivyo sehemu kubwa ya maamuzi madogo madogo yanafanywa na huyo msimamizi aliyeko katika eneo la ujenzi, (site foreman). Sasa kwa bahati mbaya kwa kuwa michoro ya mwisho ya usanifu na uhandisi haikaguliwa kuangaliwa ufanano wake kabla ya utekelezaji wa ujenzi kuanza, michoro ya uhandisi ilikuwa na makosa kidogo ambayo yalipelekea eneo fulani la nje kutoendana na michoro ya usanifu kwa kuwa ramani ya msingi(foundation plan) iliyokuwa inatumika ilikuwa ni ya michoro ya uhandisi.
Kwa bahati nzuri hilo liligunduka mapema kupitia fundi seremala na hivyo tukafanya maamuzi sahihi kuhakikisha kile kilichorukwa kinafanyika na mambo kuendelea kama yalivyokuwa yameamuliwa. Suala hili lilileta ukakasi kidogo na mshtuko kwa sababu kuna ufuatiliaji wa karibu sana wa mradi huo kwa upande wa usimamizi na picha na video kutumwa kila siku kwa wahusika. Hata hivyo hilo ni jambo ambalo lazima lingejulikana lakini kilichopelekea kuchelewa kujulikana ni kwa sababu wasimamizi walichukulia kwamba michoro yote ya kitaalamu iko sawa na inafanana hivyo walipokuwa wanafuata mmojawapo ambao ulikuwa na makosa hawakuwaza kwamba unaweza kuwa na hitilafu yoyote ndio maana hawakuona kama kuna tatizo kabisa. Lakini baadaye katika maeneo ya huku juu muda ulipofika wa kuhitaji kuzingatia mwonekanao bora kama picha zinavyotaka ndio kosa hilo likawa Dhahiri, lakini bahati nzuri likawa bado ni kosa dogo linalorekebishika.
Jambo hili ndio limepelekea mimi kuandika makala hii kwani lilinikumbusha suala ambalo nimekuwa nikiliandika hapa kwamba mchakato wa utekelezaji unapaswa kuwa unafuata utaratibu maalum uliotengenezewa kanuni. Moja kati ya hatua za mwanzoni kabisa za mchakato huo wa utekelezaji unaozingatia utaratibu maalum ulioandaliwa kwa ajili ya mradi husika wa ujenzi ni uwepo wa kikao cha kwanza cha ufundi wa kitaalamu kinachohusisha wataalamu wote ambao wamefanya michoro ya ramani za kitaalamu inayokwenda kutekelezwa kwenye ujenzi husika. Kati ya hao wataalamu muhimu kabisa ni pamoja na msanifu wa jengo au mradi, kisha mhandisi wa jengo au mradi na mhandisi wa huduma zinazojumuisha umeme, mfumo wa maji safi na maji taka ndani ya jengo au mradi mzima, kiyoyozi, umeme wa jua kama upo, mifumo ya mitandao n.k.,.
Kikao hiki cha wataalamu kitajadili michoro yote kwa kina hususan yale maeneo yote yenye changamoto na kuyadili kwa kina mwanzoni na kufikia maamuzi. Mtaalamu wa usanifu wa jengo au mradi na uhandisi wa jengo au mradi watapaswa kujadili kwa kina zaidi kila kitu kwa umakini mkubwa kuandika mapendekezo yote ya maeneo yenye utata yatakavyokwenda kufanyiwa kazi. Baada ya hapo sasa kazi inaweza kuanza ikifuata mchakato maalum wa utekelezaji ulioandaliwa na kwa ajili ya mradi husika kwa namna ulivyo. Utaratibu huu utasaidia sana kupunguza makosa na kufanikisha mradi au jengo lililofanyika katika viwango bora na vya hali ya juu sana kadiri ya namna ulivyoamuliwa katika kikao husika. Mipango mingine ya vikao vyote vinavyofuata pia pamoja na agenda zinazokwenda kujadiliwa itafanyika katika kikao cha kwanza huku ikiendelea kuboreshwa zaidi kwenye vikao vinavyofuata.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255 717 452 790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!