KILA NYUMBA/JENGO LINA GHARAMA YAKE TOFUATI.

Jambo ambalo huwa tunakutana nalo kila siku na timu yetu hapa ofisini ni watu mbalimbali hususan wanaopitia katika tovuti hii na kwingine kuuliza gharama mbalimbali za kazi za ujenzi walizokutana nazo kwenye tovuti au maeneo mengine. Hii inatokana na kwamba watu hudhani nyumba yao au mradi wao wa ujenzi unaenda kuwa kile wanachokiona na kwamba kazi hiyo au nyumba hiyo aliyokutumia ina gharama zake kamili ambazo ndizo anazokwenda kuingia yeye atakapoamua kujenga. Japokuwa katika hali ya kawaida ni sahihi mtu yeyote kufikiria hivyo lakini katika uhalisia mambo huwa hayaendi katika mstari ulionyooka hivyo.

Nilishawahi kuandika kwenye makala zilizopita kwamba majengo hayafanani kabisa, hata kama ni jengo hio hilo limejengwa sehemu nyingine bado kuna uwezekano wa gharama kutofautiana kutokana na sababu nyingi mbalimbali. Pia niliwahi kuandika kwamba huwa ni vigumu sana pia kukutana na watu wawili ambao mahitaji yao ya nyumba na vyumba vyake yakawa yanafanana kabisa bila kutofautiana chochote, kuna uwezekano wa zaidi ya asilimia 90 kwamba watu wawili watakuwa na mahitaji yanayotofautiana sana kutegemea na hali zao, mahitaji, vipaumbele na yale wanayopendelea. Utofauti huo wa kimahitaji tayari unaleta utofauti wa nyumba zao na moja kwa moja kupelekea tofauti ya gharama pia.

Sasa inapokuja kwenye utofauti wa majengo maana yake pamoja na kutajiwa gharama ya jengo ni kiasi fulani, kwanza kuna uwezekano wa zaidi ya asilimia tisini kwamba jengo lako halitafanana na hilo uliloliona lakini pia hata ikitokea limefanana bado gharama zinaweza kutofautiana kwa sababu nyingi sana mbalimbali. Hivyo pale mtu unapovutiwa na nyumba/jengo fulani kisha ukauliza gharama na kuambiwa gharama zake, bado haitakuwa sawa kuchukulia moja kwa moja kwa unakwenda kuingia gharama hizo kwa mradi wako. Gharama hizo huweza kupungua kwa sababu mbalimbali wakati mwingine hata kuongezekana kwa sababu nyingi mbalimbali pia.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *