MAAMUZI KWENYE UJENZI YANAHITAJI BUSARA NA AKILI.

Kwa kawaida sisi binadamu huwa tuna njia mbili tunazotumia kwenye kufikia maamuzi ambazo ni kufanya maamuzi kwa kutumia hisia au kufanya maamuzi kwa kutumia akili. Njia ya kufanya maamuzi kwa kutumia hisia huwa ndio njia rahisi inayokuja yenyewe kwa haraka na ndio yenye nguvu kwa watu wengi sana. Hata hivyo wanasaikolojia wengi wanaamini kwamba binadamu wote wanafanya maamuzi kwa kutumia hisia kisha wanayohalalisha kwa kutumia akili, yaani wanatafuta sababu ya kuyahalalisha au kuyatetea kwamba ndio maamuzi sahihi.

Hata hivyo binadamu tumeumbwa kutumia hisia zaidi kwa sababu ndio asili iliyopo ndani yetu kwa miaka sana ukilinganisha na weledi wa akili ambao ni kama mazoea mapya ndani ya binadamu. Hivyo uwezekano wa mtu kufanya maamuzi kwa kutumia hisia ni mkubwa sana ukilinganisha na utumiaji wa akili. Lakini pamoja na hayo maamuzi ya kutumia hisia pasipo kuhusisha akili ambapo itataka kwenda zaidi njia ngumu ni mara chache huwa maamuzi sahihi kwani akili yako inafanya kukulinda na hatari lakini ambayo inatokana na hofu isiyo na maana tena kwa zama hizi. Maamuzi ya kutumia hisia mara nyingi humpeleka mtu kwenye kufanya maamuzi rahisi kwake, kupenda starehe, kupenda njia za mkato, kupenda rahisi bila kujali madhara yake, kuwa mvivu wa kufanya na kufikiri, kufanya mambo kwa upendeleo ili kujinufaisha binafsi kwa sababu mbalimbali n.k.,

Kutumia busara na akili maana yake ni kufanya maamuzi sahihi wakati wote bila kujali kama yanaumiza au hayaumizi na bila kujali kama yanafurahisha watu wako wa karibu, muhimu yawe ndio maamuzi sahihi au kwa maana nyingine ndio maamuzi yenye mwisho mwema ambao hautakuwa na majuto. Lakini changamoto kubwa tuliyonayo ni kwamba hayo sio maamuzi ambayo hufanyika bali watu huendelea kuwa watumwa wa hisia zao kwa 100% kwa kuendelea kufanya maamuzi yasiyo na mwisho sahihi au yasiyofaa kwa sababu ya kukwepa maumivu au kutafuta urahisi.

Kwa mfano mtu anaweza kutakiwa aanze kwanza kufanya michoro ya ramani kabla ya kuanza ujenzi kisha akapewa uhuru wa kuamua lakini akaishia kwenda kutafuta fundi wasaidiane kutengeneza ramani ambayo haijazingatia taratibu sahihi za kitaaluma ili kuepuka maumivu ya kutoa fedha kulipia michoro ya ramani. Hayo tunasema sio maamuzi ya busara kwa sababu fedha anazokwenda kutumia kwenye ujenzi ni nyingi sana, pengine hata zaidi ya mara 300 ya hizo gharama za michoro ya ramani anazoambiwa. Mwisho anafanikiwa kujenga jengo ambalo lina michoro ya ramani ambayo iko chini ya viwango na jengo hilo kwa muonekano wake na mipangilio ya ndani ya jengo inakuwa isiyovutia kabisa. Pesa nyingi zinatumika kujenga jengo ambalo mwishoni litachukiwa kuanzia na mwenye jengo mwenyewe mpaka watumiaji wa jengo hilo.

Mfano mwingine ni kwenye vifaa vya ujenzi na ufundi na usimamizi wa jengo. Mtu kwa kushindwa kufanya maamuzi ya busara katika kununua vifaa au kutofanya ufuatiliaji wa kina anaishia kununua vifaa feki au vilivyo chini ya kiwango na kuwaachia usimamizi wa mradi watu wasio na uwezo wa kutosha na hayo yote kuishia kupoteza kwa kila upande. Mteja anakuwa amepotezewa gharama zake na muda huku mtaalamu husika akiwa ameharibu sifa yake sokoni pamoja na mahusiano yake na mteja husika na watu wake wa karibu.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *