KUFANYA KAZI BORA YA USANIFU WA JENGO INAHITAJI MUDA WA KUTOSHA KUUMIZA AKILI.

Kwa mtu yeyote mwenye akili ya kiuchunguzi katika kufuatilia mambo na kuelewa kwa kina anakubaliana na ukweli kwamba kitu chochote ili kifanyike kwa ubora na umakini huhitaji uwekezaji wa muda na akili kubwa ya mtu mwenye uwezo mkubwa katika eneo husika. Sasa tunapokuja katika timu nzima ya ushauri wa kitaalamu kwenye jengo na kutengeneza michoro lile wazo zima la mpangilio, nafasi na matumizi ya jengo hufanywa na msanifu wa jengo, yaani msanifu wa jengo ndiye anahusika na matumizi ya jengo na maamuzi ya namna maeneo mengine katika jengo yatafanyika ili yasiathiri matumizi na mpangilio wa jengo kimuonekano.

Hivyo sasa kazi hiyo ya kubuni na kusanifu jengo kuanzia wakati halipo kabisa mpaka kuweza kulifikisha katika eneo ambapo linakuwa lina kila kitu ndani na mpangilio sahihi wa nafasi na vyumba vyote kulingana na uhusiano wa kimatumizi ni kazi inayohitaji utulivu na ubunifu mkubwa. Ikiwa kazi hiyo haitapewa muda wa kutosha na ubunifu wa kiakili wa kutosha katika kuja na wazo sahihi na mambo mengine yote basi kazi hiyo huenda ikafanyika katika viwango duni kuanzia kimpangilio mpaka kumuonekano. Kwa maana hiyo ili kazi hiyo iwe ni kazi bora yenye ubunifu kuanzia kimpangilio mpaka muonekano unaovutia na kusisimua lakini wenye mantiki na maana kitaaluma inatakiwa kazi husika ipewe muda wa kutosha na uzoefu mkubwa katika taaluma ya usanifu majengo kwa mradi husika.

Unapoona jengo zuri lenye kupendeza macho na lililopangiliwa vizuri sana kwa ndani kwa kuanzia uhusiano uliopo kati ya nafasi na vyumba, mwanga wa asili wa kutosha ndani ya jengo, hewa safi na nyepesi ya kutosheleza, umaridadi wa vipengele mbalimbali vya ujenzi kama kuta, paa na mipangilio mingine bora ndani ya jengo unapaswa kujua kwamba kuna kazi kubwa sana ya kutafiti na kuumiza akili imefanyika kufikia hapo. Sasa ili mtu uweze kufanya kazi nyingine ya viwango hivyo au zaidi ya hapo kunahitajika kazi kubwa ya kutafiti, kujifunza zaidi kutoka kwenye miradi mingine na kuweka kazi kubwa sana ya kufikiri na kujadili kama timu kuweza kufanikisha kazi husika.

Kama hakutakuwa na kipaumbele katika kuwekeza muda na akili basi thamani ya kile kinachofanyika haiwezi kuwa kubwa kama jinsi ambavyo ingekuwa ikiwa kungekuwa na uwekezaji huo. Hivyo ni muhimu kuzingatia hilo ikiwa mtu unahitaji au unavutiwa na kazi ambayo inaonekana ni nzuri sana na ya viwango vya juu sana.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *