MWISHO WA MRADI WA UJENZI UTAGUNDUA HOFU YAKO HAIKUPASWA KUWA GHARAMA.

Kutokana na uhaba na umuhimu wake karibu kila mtu anapoamua kuingia kwenye mradi wa ujenzi kabla ya kuanza kitu anachofikiria sana kwenye akili yake ni gharama za ujenzi. Ni kweli kwamba gharama za ujenzi ndio kitu muhimu cha kuangalia kwa sababu kwanza ndio zinazoamua kama mradi ujengwe au usijengwe na hata kuamua mradi ujengwe kwa ukubwa gani au uhusishe vitu gani ndani yake. Hivyo kuweka umakini kwenye gharama na namna ya kudhibiti gharama ni jambo muhimu sana lakini ni jambo linalotakiwa kufanyika kwa makini sana na kwa mbinu sahihi.

Hata hivyo baada ya mradi wa ujenzi kufika mwisho utakachokuja kugundua ni kwamba kuna mambo mengine mengi yalipaswa kupewa kipaumbele tofauti na gharama lakini hayakupewa kipaumbele inavyostahili kwa sababu mkazo wote ulikwenda kwenye gharama na pengine hilo limesababisha changamoto pia. Yaani pengine kuweka umakini mkubwa kwenye gharama pekee imekuwa sehemu ya tatizo kwa kufanya maamuzi yasiyo sahihi. Kwa sababu kwanza mara nyingi gharama za ujenzi huongezeka zaidi kuzidi yale makadirio yaliyofanyika mwanzoni kabla ya ujenzi kuanza hivyo hofu ya gharama inakuwa ilikuwa haina maana sana lakini pia utofauti wa gharama ni mdogo sana kulinganisha na umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi ya vifaa au ufundi unaoenda kuwekwa kwenye kazi husika. Ni sahihi na kufurahia kununua simu ya bei rahisi lakini inakuja kuishia kukusumbua sana baada ya muda kidogo kiasi kwamba unaona kwamba usumbufu huo ni mkubwa sana ukilinganisha na ile gharama uliyokwepa ili kupata simu nzuri.

Baada ya kukutana na usumbufu, uchelewaji na kukosekana kwa ubora uliotarajia katika kazi hiyo ya ujenzi ndipo unagundua kwamba ulipaswa kuweka umakini mkubwa zaidi kwenye katika kufanya maamuzi sahihi ya vifaa na huduma ya ufundi kuliko ile nguvu uliyoweka kwenye kupambania bei nafuu. Mradi wa ujenzi unahusisha mambo mengi sana ndani yake na unakuja na gharama nyingi na kubwa sana ambapo kama kuna uharibifu wa aina yoyote ile hasara yake mara nyingi huwa ni kubwa sana ukilinganisha na kile watu wanachoangalia. Mtazamo wa mwanzoni na mwishoni wa mtu yeyote anayefanya mradi wa ujenzi huwa ni tofauti sana kutokana na yale aliyopitia katika mchakato mzima. Hii ni kwa sababu mwanzoni mtu huwaza gharama tu bila kufikiria kingine chochote kinachoweza kutoka katikati ya safari lakini mwishoni huja kugundua kwamba kuna mambo mengine mengi alipaswa kuyapa kipaumbele, na kama hasara aliyopata ni kubwa sana basi huishia kwenye majuto sana.

Kwa hivyo ni muhimu sana mtu unapoanza kufanya mradi wa ujenzi katika ya mwanzo kabisa kuhakikisha unafahamu ni mambo gani ya kuyapa kipaumbele kikubwa mwanzoni ili angalau kwa sehemu kubwa upunguze makosa hasa kama ndio mara yake ya kwanza kufanya mradi wa ujenzi.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *