UZURI NA UBORA WA RAMANI YA UJENZI UKO KWENYE MABORESHO.

Katika kazi zinazohusisha kufikiria na kutumia akili ili kufanya kazi bora na yenye ubunifu wa hali ya juu, mara nyingi toleo la kwanza huwa na mapungufu aidha kidogo au zaidi. Lakini mapungufu hayo yanapojadiliwa na kufanyiwa maamuzi toleo la pili huwa na ubora zaidi kuliko la kwanza kwa kiasi kikubwa kwa sababu timu nzima inayofanya kujadili kazi hiyo inakuwa imeingiza mchango wake wa mawazo kutoka kwenye uzoefu. Lakini hata hivyo bado kunaweza kuhitajika pia toleo la tatu na la nne pengine hata mpaka la tano kulingana na kuelewana kwa wahusika au changamoto iliyopo kwenye kazi hiyo.

Sasa unapokuja kwenye kazi ya kubuni ramani ya ujenzi mchezo huwa ndio huo, yaani kazi ikifanywa tu mara moja bila kujadiliwa kwa kina na kuikosoa ili kuongeza ubunifu bado huenda ikawa haipo katika viwango vya juu sana. Lakini kazi hiyo inapoingizwa kwenye mjadala wa pamoja na kujadiliwa na kwa kina na kutolewa mapendekezo tolea linalofuata la kazi hiyo huwa bora zaidi na lililozingatia mambo mengi zaidi muhimu. Hii ni kwa sababu hata mtaalamu wa usanifu majengo mwenyewe hujikuta akijongeza zaidi na zaidi kuhakikisha anafanya kwa ubora yale yanayojadiliwa huku akijua kwamba baada ya kukamilisha kazi itawekwa tena kwenye mjadala na kukosolewa.

Hivyo kwa faida ya mchango wa wengi kwenye kazi hiyo sambamba na umakini wa mtaalamu wa kusanifu unaokuwa umesababishwa na kukosolewa au kujua kwamba kazi yake inakwenda kuhukumiwa basi kazi husika inawekwa ubunifu wa hali juu kuzingatia yote muhimu yanayohitajika au yaliyopendekezwa. Hiyo ndio sababu kwa majengo mengi kwa nchi nyingine hasa zile zilizokomaa kisiasa na kupiga hatua kimaendeleo kazi hizi hukosolewa na watu mbalimbali wakiwemo waandishi katika magazeti na majarida yanayosomwa sana. Lakini hata kwa miradi isiyokosolewa na umma inaweza kuwa nzuri zaidi inapopata ukosoaji na kuwa bora kupitia maboresho yanayofanywa kuziba yale maeneo yaliyopata ukosoaji unaostahili.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *