KUSAJILI MRADI WA UJENZI KWENYE BODI ZA UJENZI NI GHARAMA KUBWA.

Moja kati ya maeneo ambayo wateja wengi wa miradi ya ujenzi huwa wanakutana na mzigo ambao huhisi unawaelemea ni kwenye kusajili mradi wa ujenzi katika bodi za ujenzi. Mara nyingi mtu anapoamua kufuatilia kibali cha ujenzi hukutana na changamoto kiasi lakini mwishowe hukamilisha kwa kulipia gharama ambazo kwa sehemu kubwa huona kama sio changamoto sana. Lakini kazi huja pale ambapo anakuwa anahitaji kuwa na bango la ujenzi na kuhitaji kusajili mradi husika katika bodi mbalimbali za ushauri wa kitaalamu katika ujenzi.

Kinachopelekea gharama hizi kuwa kubwa kuliko mategemeo ni sababu kama tatu hivi. Kwanza kabisa ni kwamba ziko bodi kuu tatu zinazoshughulika na miradi ya ujenzi ukiondoa taasisi nyingine ambazo hazihusiki moja kwa moja. Bodi hizo kuu tatu ni ya kwanza ni bodi ya wasanifu majengo na wakadiri au Architects and Quantity Surveyors Registration Board(AQRB), pili kuna bodi ya wahandisi au Engineers Registration Board(ERB) na tatu ni bodi ya wakandarasi au Contractors Registration Board(CRB). Sasa bodi zote hizi kila moja inajitegemea na ina taratibu zake, sheria zake na gharama zake tofauti za kupata usajili kwao. Na ikiwa unachukua kibali cha jengo bodi ya AQRB ambayo inahusika na wataalamu wa aina mbili inatoa usajili wa mradi katika fani mbili tofauti.

Ukiachana na gharama za kusajili mradi pia utakutana na gharama za kuwalipa hizo kampuni kwa ajili ya huduma yao ya usimamizi wa mradi husika katika hatua hiyo ya usimamizi wa mradi iwe watasimamia au hawatasimamia. Sasa kulipia gharama za serikali kwa usajili wa mradi kwa angalau fani nne tofauti halafu bado unawalipa hao wataalamu wenye makampuni yanayotoa huduma hizo mwenyewe unaweza kujiona gharama zake zinaweza kufika mbali kiasi. Hivyo ni muhimu kujiandaa kisaikolojia na gharama hizi pale unapofikiria kusajili mradi wa ujenzi katika bodi hizi za ujenzi vinginevyo labda kama kuna njia nyingine uliyoiandaa kupitia. Wastani wa bei kwa ujumla tunaweza kusema ikiwa utasajali mradi huo kwa bodi zote nne nilizozitaja hapo juu kwa mradi wa kiwango cha chini kabisa basi ni wastani wa kuaniza milioni tano na kuendelea.

Hata hivyo miradi inayosajiliwa kwenye bodi za ujenzi kwa upande wa nyumba ya kuishi ni ile ya ghorofa peke yake, ikiwa jengo lako sio la gharama huwa halina ulazima wa kusajiliwa kwenye bodi hizi za ujenzi badala yake unaweza kuendelea na ujenzi bila kuletewa usumbufu wowote mara tu baada ya kupata kibali cha ujenzi kutoka kwenye halmashauri ya mji/jiji/manispaa husika. Lakini jengo linapokuwa ni la gharama na hasa kama liko katika eneo la mji/manispaa/jiji basi unaweza kukutana na usumbufu mwingi sana mpaka kutakiwa kusajili mradi katika bodi hizi za ujenzi.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *