MRADI WA UJENZI UNAHITAJI USIMAMIZI MKALI SANA LAKINI BADO UTAKUSHANGAZA.

Katika hali ya kawaida baadhi ya watu wanapoangalia au kufikiria kuhusu mradi wa ujenzi huwa wanauona kwa namna ya kawaida na kuufikiria katika namna rahisi sana na iliyonyooka. Ni mpaka pale mtu anapokuja kufanya mradi wa ujenzi ndipo anagundua kwamba mradi wa ujenzi katika utekelezaji wake sio wa kawaida kama unavyofikirika au kuonekana kwa nje bali ni tata sana kuanzia usimamizi wake mpaka gharama, na hasa usimamizi wa gharama, ufundi na kudhibiti ubora. Kuna mambo mengi sana yanapaswa kudhibitiwa na kuendewa kwa akili sana ili kuweza kufanikisha mradi kwa usahihi kiufundi, kwa muda uliopangwa na kwa bajeti iliyopangwa.

Hata hivyo pamoja na kujitahidi sana kwa kutumia mbinu mbalimbali za usimamizi wa miradi ya ujenzi hata kama mradi wa ujenzi sio mkubwa sana bado kuna namna nyingi sana utakushangaza kwa kuja na changamoto usizozitarajia. Changamoto huweza kuwa na usumbufu zaidi na yenye gharama kubwa zaidi ikiwa mradi husika haujahusisha ushauri wa kitaalamu au usimamizi wa washauri wa kitaalamu. Hii ni kwa sababu miradi ya ujenzi ina mambo mengi ambayo hayapewi uzito sana kwa mtazamo wa juu juu lakini hupunguza sana thamani ya jengo pale yanaposhindwa kufanyika kitaalamu. Mambo yasiyotarajiwa na changamoto zisizotarajiwa katika mradi wowote wa ujenzi huwa ni lazima kutokea hata kama kutakuwa na umakini mkali kiasi gani katika udhibiti.

Lakini pamoja na changamoto zote hizi bado kuna njia za kupunguza sana changamoto na kuhakikisha matokeo ya mwisho yanakuwa yenye ubora sana. Hili litafanikishwa kwa kwanza kuhakikisha mradi una usimamizi au kukaguliwa mara kwa mara na wataalamu wa fani husika za usanifu majengo na uhandisi mihimili. Lakini muhimu kuliko yote ni kuweka mfumo wa utekelezaji wa mradi husika ambao umeshafanyiwa kazi na kuboreshwa sana kiasi kwamba changamoto zote za kushtukiza zinazotokea mara kwa mara katika miradi mbalimbali na kujirudia katika miradi mingine zinafahamika na kudhibitiwa na mfumo. Mfumo wa utekelezaji umejumuisha suluhisho la changamoto nyingi sana zinazoweza kujitokeza wakati mradi unaendelea lakini pia kuandaa mazingira mazuri na sahihi sana ya kukabiliana na changamoto mpya kabisa ambayo haijawahi kutokea ikajumuishwa kwenye mfumo na mara baada ya kutatuliwa itaongezwa kwenye mfumo huo wa utekelezaji ili izidi kuuboresha zaidi kwa manufaa ya miradi zaidi inayokuja.

Karibuni sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *