MTAALAMU ALIYEFANYA UBUNIFU WA JENGO NA MICHORO USIMWACHIE.

Baadhi ya watu baada ya kukamilisha hatua ya michoro ya ramani huchukua michoro hiyo na kuondoka nayo kisha kwenda kutafuta watu wa kujenga na yeye mwenyewe kusimamia ujenzi au kutafuta fundi wa kusimamia ujenzi. Wakati mwingine hufanya hivi baada ya kuvunja mahusiano na mtaalamu aliyebuni na kuchora jengo hilo au kwa kwenda kufanyia kazi hiyo ya ujenzi mbali kabisa na uwezekano wa kumpata mtaalamu huyo bila kujua kwamba kuna uwezekano mkubwa atamhitaji kwa sehemu muhimu sana ya aidha marekebisho au ufafanuzi.

Changamoto inayopelekea kumhitaji huenda ikatokea mara tu wakati amejikuta analazimika kuchukua kibali cha ujenzi ambapo baada ya kupeleka michoro hiyo katika idara husika za halmashauri ya mji/manispaa/jiji akakuta kwamba kuna sheria tofauti na hivyo michoro inatakiwa kufanyia marekebisho ili ipitishwe na kupewa kibali. Jambo hilo linaanza kuwa gumu kwa sababu anashindwa kufanya mabadiliko hayo lakini hata anapopata mtaalamu mwingine ambaye yuko tayari kufanya kazi hiyo anakuwa hana hilo file katika nakala tete ili alifungue na kufanya marekebisho na badala yake analazimika kufanya kazi upya na gharama zake zinakuwa ni nyingine tena kama hizo.

Au changamoto nyingine inakuwa kwamba kazi husika inashindwa kuenea kwa usahihi kwenye eneo inapojengwa nyumba hiyo na hivyo kuhitaji mabadiliko kidogo lakini hilo linashindikana. Lakini muhimu kabisa ni pale ambapo mteja mwenyewe unapogundua kwamba kuna mabadiliko unayohitaji yafanyike kwani kuna mahitaji ambayo umeyahitaji baada ya kuangalia michoro ya ramani kwa umakini zaidi hivyo umelazimika kuhitaji maboresho. Hata hivyo kwa kuwa mtu huyo hapatikani na mtu mwingine atakuchaji upya tena kwa kazi hiyo basi itakuwa ni gharama kubwa kwako na huenda kazi yake isiendane vizuri na hiyo iliyokuwa imefanyika.

Mwisho kabisa ni ikiwa jengo ni la ghorofa na linahitaji kusajiliwa kwenye bodi za ujenzi ikiwa umebadilisha mtaalamu huwa inatakiwa yule mtaalamu wa kwanza kuandika barua ya kuridhia kazi hiyo iendelee katika hatua ya usimamizi wa ujenzi na mtaalamu mwingine au kampuni nyingine. Ikiwa mtaalamu huyo wa kwanza hajaandika barua ya kuridhia hilo huenda ukakutana na usumbufu mkubwa au kuhitajika kutumia gharama kubwa kupata njia mbadala.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *