RAMANI YA KIWANJA INAYOTUMIKA NI ILE AMBAYO NI RASMI ILIYOFANYWA NA MPIMAJI.

Kwa miaka ya siku hizi sehemu kubwa ya ardhi iliyopo ndani ya halmashauri za miji/manispaa/majiji zimepimwa au tayari kuna ramani ya kiwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali hususan makazi. Kazi hii ya upimaji sio kazi inayofanywa kiholela au kiurahisi tu na mtu yeyote bali ni kazi ya kitaalamu inayofanywa na watu wenye taaluma husika wanaofahamika kwa majina ya kitaalamu kama “land surveyors” au wapimaji. Hata hivyo jina “land surveyors” linaweza kuwa kama limepitwa na wakati kwa sababu wataalamu hawa hawafanyi upimaji kwenye ardhi pekee bali hata majini na hewani.

Wataalamu hawa wa upimaji wana taratibu zao za taaluma yao na ndio hutoa ramani hizi katika vipimo vyenye usahihi wa hali ya juu sana na ramani zenyewe zikiwa katika usahihi mkubwa. Hakuna mtaalamu mwingine yeyote mwenye uwezo wa kufikia usahihi wa hali ya juu kiasi hicho wa upimaji kwa sababu anakosa maarifa sahihi na vifaa vya kufanya hayo. Lakini kwa sababu mbalimbali unakutana na viwanja ambavyo aidha havijapimwa au vimepimwa lakini taarifa za vipimo hivyo haipatikani kwa sababu mbalimbali aidha kuharibika au kupotea. Katika hali kama hii mtaalamu wa kuchora jengo atahitajika kufanya vipimo mwenyewe ili aweze kufanya kazi ya michoro.

Hata hivyo inapotokea kwamba ramani ya kiwanja inaweza kupatikana basi inatakiwa ipatikane na kutumika hiyo kwa sababu ndio ramani yenye usahihi mkubwa na inayokwenda kukubalika na kutambulika kwenye halmashauri husika. Hili ni muhimu kwa sababu watu wengi hupenda kuamini kwamba mtaalamu anayechora ramani ndiye mwenye mamlaka makubwa na ya mwisho katika miradi ya ujenzi ikiwa ni pamoja na kuchukua vipimo sahhi. Lakini ni vigumu sana ramani ya kiwanja kilichopimwa na mtaalamu wa upimaji ikafanana kwa usahihi kabisa na ramani iliyofanywa na mtaalamu wa usanifu majengo ambaye anachukua vipimo kikawaida.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *