KIBALI CHA UJENZI WA NYUMBA KIAMBATANE NA KIBALI CHA UZIO AU FENSI.

Kwa maeneo ya mjini sasa ni wazi kwamba muamko wa watu kufuatilia vibali vya ujenzi kwa majengo na nyumba zao umekuwa mkubwa sana. Watu wengi sasa kila wanapofikiria kuhusu kujenga kwenye maeneo ambayo yako chini ya halmashauri za miji, manispaa na majiji wamekuwa wanafikiria kwanza kuhusu kibali cha ujenzi na hata usajili wa kwenye mamlaka nyingine pia. Hizi ni habari njema sana kwa sababu tabia hii inasaidia sana katika kuhakikisha kwamba miji inapangika vizuri na watu wanajenga kwa kuzingatia sheria na taratibu kitu kinachosaida ujenzi kuwa bora na thamani ya makazi na miji kuongezeka sana kadiri siku zinavyoendelea mbele.

Hata hivyo kwa miaka ya sasa tofauti na zamani kwa sababu zaidi za kiusalama na faragha huwezi kujenga nyumba yoyote ya thamani bila kufikiria ujenzi wa uzio au fensi. Tena watu wengi siku hizi huanza kabisa kujenga kwanza uzio kabla ya kuanza ujenzi mkuu wa nyumba yenyewe kwa sababu zile zile za kiusalama na faragha hata wakati ujenzi unaendelea. Hata hivyo sio jambo la ajabu kwani uzio au fensi huongeza sana thamani ya nyumba ukilinganisha na nyumba isiyo na uzio/fensi. Lakini kwa mujibu wa taratibu za mamlaka za miji, manispaa na majiji uzio nao unahitaji kupatia kibali kutoka halmashauri baada ya kuwasilisha michoro iliyotimiza vigezo na masharti ya ujenzi wa uzio kama ilivyokuwa kwa ujenzi wa nyumba. Baadhi ya halmashauri za manispaa zimefikia hatua huwa zinachunguza hata uzio/fensi zilizojengwa bila kubali na kutoza adhabu kwa wahusika hata kama fensi hiyo ilijengwa miaka iliyopita.

Hivyo ni muda muafaka sasa pale mtu anapofikiria kuhusu kuanza kufanya michoro ya ramani ya nyumba yake ajumuishe michoro ya ramani za fensi ili anapopewa kibali cha ujenzi kiwe kimejumuisha ujenzi wa fensi ndani yake. Kufanya hivi itasaidia sana kurahisisha zoezi la kibali cha fensi na hata kupunguza gharama zake kwa kiasi kikubwa sana. Unapompa mchoraji kazi ya kufanya usanifu wa jengo lake ukamwambia kazi hiyo ni pamoja na ramani za fensi zinazojumuishwa kwenye kibali cha ujenzi atakufanyia kazi hiyo kwa pamoja kwa gharama nafuu ukilinganisha na pale ambapo utafanya ramani ya nyumba halafu baadaye uje tena ufanye upya ramani ya fensi.

Kwa maana hiyo kwa sasa usifikirie kabisa kufanya ramani ya nyumba bila kuijumuisha na ramani ya fensi pamoja na geti kwani itakuokolea gharama na kukupunguzia usumbufu mkubwa wa kufanya kazi mara mbili.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *