KIBALI CHA UJENZI KINACHUKUA MUDA GANI KWA MCHAKATO MZIMA KUKAMILIKA?

Mamlaka mbalimbali za serikali pamoja na nyingine zisizo na uhusiano wa moja kwa moja na serikali zimeendelea kuboreshwa na kutanuka zaidi katika kuwapelekea watu huduma karibu sana na wao ili pia kuweza kudhibiti mambo yafanyike kwa kufuata utaratibu uliowekwa. Kutokana na kutanuka sana kwa mamlaka hizi basi watu wengi sana siku wanajitahidi kujiongeza kwa kufuatilia ili kupata kibali cha ujenzi kwa aina ya ujenzi wowote wanaoanzisha au kuendeleza. Hii ni hatua nzuri sana na ya kupongezwa kwani kwa watu kufuatilia kibali cha ujenzi maana yake ni ujenzi kufanyika kwa kufuata kanuni za kitaalamu hivyo kupelekea kuwa na majengo yenye ubora na mipangilio sahihi ya miji.

Hata hivyo kati ya maswali mengi ambayo watu hujiuliza na kukosa ufafanuzi wa hapo hapo ni kuhusu namna na vigezo na masharti ya kupata kibali cha ujenzi na kwamba kibali hicho kinachukua muda gani. Kwanza kabisa tukianza na hili la vigezo na masharti ya kupata kibali cha ujenzi; sharti kuu la kupata kibali cha ujenzi ni kuwa na michoro ya ramani iliyochorwa kitaalamu na wasanifu majengo na wahandisi waliosajiliwa na bodi husika za ujenzi na kupiga mihuri yao rasmi pamoja na nakala ya hati ya kiwanja husika kinachojengwa jengo hilo. Kwa kawaida michoro hiyo huwa katika seti saba na huko halmashauri za miji, manispaa na majiji mara nyingi huhitaji nakala tatu za michoro hiyo zilizoidhinishwa na mtaalamu anayetambulika na bodi husika.

Sasa kuhusu muda ambao mchakato mzima wa kibali unachukua tangu kupelekwa kwa maombi ya kibali yaliyoambatana na michoro ya ramani ya ujenzi inayokwenda kujengwa unategemea na vitu kadhaa. Kwanza ni michoro husika kuwa imetimiza vigezo vilivyowekwa na halmashauri husika na kisha matumizi ya eneo husika kwa mujibu wa mipango ya idara za mipango miji yawe yanaendana na michoro ya ramani inachopendekeza. Ikiwa vigezo hivyo viwili tajwa hapo juu vimezingatiwa basi kibali cha ujenzi hakina tena kizuizi lakini sasa suala la muda gani kitapatikana inategemea na mambo makubwa mawili.

Jambo la kwanza ni faili lenye michoro hiyo ya ramani inayoombewa kibali kumaliza mzunguko katika idara zote za halmashauri ya mji, manispaa au jiji husika na jambo la pili ni kikao cha halmashauri husika kinakaa siku gani au kila baada ya muda gani. Faili kumaliza mzunguko na suala la kulifuatilia lipite kwenye idara zote zinazotakiwa za halmashauri kama vile idara ya mipango miji, idara ya mazingira, idara ya afya, idara za ujenzi n.k., Faili likipitishwa kwenye idara zote na kwa mafanikio zoezi ambalo linaweza kumalizika hata ndani ya siku moja au mbili basi kinachokuwa kimebakia ili kupata kibali ni kikao cha wataalamu wa idara zote za ujenzi kujadili vibali hivyo kisha kuandikwa na kukabidhiwa kwa wahusika.

Kuhusu vikao hivyo vya halmashauri hutofautiana kati ya halmashauri moja na nyingine. Kuna halmashauri ambazo huwa kuna kikao cha kujadili vibali vya ujenzi kila wiki kama vile halmashauri ya manispaa ya Kinondoni, lakini kuna halmashauri hukaa vikao mara moja kwa kila wiki mbili kutegemeana na mipango yao wenyewe. Hivyo faili husika linapomaliza mzunguko na kukutana na kikao maana yake kibali cha ujenzi kimepatikana tayari kwani ni vigumu sana kwa kikao cha kijadili vibali kuzuia kibali kwa faili ambalo limemaliza mzunguko kwenye idara zote na kutimiza vigezo vya kuingizwa kwenye kikao. Mabadiliko haya ya vikao kufanyika mara kwa mara sana yalifanyika kwenye serikali ya awamu ya tano ambayo iliwaondoa baraza la madiwani ambao walisababisha vikao hivi kuchelewa sana na kufanyika aidha mara moja kwa mwezi au mara moja baada ya miezi mitatu kwa halmashauri nyingine.

Hivyo kibali cha ujenzi sio kitu kitakachokuchukua muda mrefu ilimradi tu unafanya kazi kwa kufuata taratibu zote za kitaalamu na unafahamu au kuwa makini na taratibu zote zilizowekwa na mamlaka husika.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *