USALAMA PEKEE KWENYE UJENZI NI KUZINGATIA KUFANYA KAZI NA WATU WAAMINIFU.

Kadiri ninavyoendelea kufanya usimamizi wa miradi ya ujenzi na kujifunza zaidi na zaidi na kufanya uchunguzi wa kina ndivyo ninavyozidi kushawishika kwamba suala la kufanya kazi na watu waaminifu haliepukiki ikiwa kweli unahitaji kukamilisha mradi wenye thamani kubwa. Ni kweli kabisa na ni muhimu sana kudhibiti uharibifu na ubadhirifu wa namna mbalimbali katika eneo la ujenzi siku zote lakini kwanza ya yote hakikisha unatafuta kufanya kazi na watu wenye viwango vya juu kabisa vya uaminifu. Kufanya kazi na watu wasiokuwa waaminifu lazima itakugharimu sana kwa sababu hata kama una mfumo imara kiasi gani watu wana akili sana za kutosha kuchakachua na kufanikisha agenda zao ambazo zitaathiri ubora wa kazi yako.

Ni kweli kwamba mifumo thabiti ya ufuatiliaji na kutoa adhabu kali na zawadi vinasaidia sana kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya kukosekana kwa uaminifu kwenye eneo la ujenzi lakini hilo sio tu kwamba halitatui tatizo kwa 100% lakini pia linasababisha watu wasio waaminifu kubadili mbinu na kutumia mbinu usiyoijua. Suala la kukosekana kwa uaminifu kwa watu ni tabia, na kama unavyojua nguvu ya tabia za watu. Tumekaa na watu mbalimbali wasio waaminifu tukiamini watabadilika kwa kuwaonya na kuwaelekeza lakini hali imezidi kuwa mbaya zaidi na zaidi na kujikuta unajuta kwa nini uliendelea kuwaacha tangu mwanzoni ulipogundua wana tabia hizo.

Hivyo ni muhimu sana kuzingatia kwamba mtu asiye mwaminifu hafai kuendelea kupewa nafasi hata kwa siku moja zaidi, mtu akishagundulika sio mwaminifu anapaswa kuondolewa mara moja na kutorudishwa tena kwa sababu ataendelea na tabia hiyo na wala hataiacha kamwe. Hakuna namna bora ya kumdhibiti mtu aliyekosa uaminifu zaidi ya kumwondoa au kumfukuza kabisa na kutojaribu kumsikiliza tena. Majuto ni mjukuu, mara nyingi utakuja kuona umuhimu wa kufanya maamuzi mapema ukiwa umeshachelewa na wakati huo unajutia.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *