UJENZI WAKATI WA MVUA.

Ni imani iliyoenea sana kwamba wakati wa mvua shughuli za ujenzi huwa zinasimama kupisha kipindi cha mvua kumalizika kwanza ndipo ujenzi kuendelea. Hivyo watu wengi wanaamini kwamba kipindi cha mvua huwa hakuna ujenzi hivyo watu husubiri mpaka kipindi ambacho mvua zimekwisha. Dhana hii tunaweza kusema kwamba ina ukweli kidogo sana kwa sasa na ilikuwa na ukweli zaidi miaka iliyopita lakini pia kwa baadhi ya maeneo machache bado ina ukweli kwa kiasi fulani. Kimsingi dhana hii inategemea na vitu vingi na maeneo.

Kwanza kabisa kwa sehemu mvua sio kwamba huwa inazuia ujenzi kufanyika lakini zaidi huwa inazuia vifaa vya ujenzi kufika katika eneo la ujenzi kutokana na ubovu wa barabara na miundombinu nyingine za barabara kwa ujumla kitu kinachopelekea kazi ya ujenzi kusimama. Lakini pia wakati wa mwanzoni kwenye kuchimba msingi wa jengo ikiwa kuna mvua kubwa mitaro na mashimo ya kwenye msingi wa jengo huweza kujaa maji na kuleta usumbufu mkubwa katika ujenzi kama vile kumwaga zege la kwenye msingi, kujenga kuta za kwenye msingi na kuseti nguzo za jengo kwenye msingi hivyo kusababisha shughuli hizo kudorora.

Lakini ikiwa mvua haijanyesha kwa siku tatu au imenyesha lakini kwa kiwango cha kawaida na sio ile mvua kubwa kabisa, basi bado suala la kuchimba msingi wa jengo na shughuli za kwenye msingi wa jengo kama vile kujenga kumwaga zege la kwenye msingi, kujenga kuta za kwenye msingi na hata kuseti na kumwaga nguzo za kwenye msingi bado sio changamoto sana. Changamoto kubwa pekee ni mvua kubwa wakati wa kuchimba msingi wa jengo na miundombinu mibovu sana ya barabara wakati wa kupeleka vifaa vya ujenzi katika eneo la ujenzi. Changamoto nyingine ni baadhi ya vifaa vinavyoweza kuathiriwa na unyevu au maji kuharibika, lakini hili lina namna nyingi za kuzuia, kuepuka na kuhifadhi hivyo changamoto yake sio kubwa.

Tofauti na hapo mvua sio tatizo sana wakati wa ujenzi kwani hata kama kuna mvua mara nyingi huwezi kukuta inayesha siku nzima na siku zote bali hunyesha na kuacha na kuruhusu shughuli kuendelea. Kwa kesi ya ubovu wa miundombinu ya barabara hiyo kwa sehemu kubwa ilikuwa ni changamoto ya zamani na kwa sasa ni changamoto kwenye baadhi ya maeneo lakini maeneo mengi na hususan ya mjini bado hiyo sio changamoto kubwa kwani inatokea kwa nadra sana na kwa baadhi ya maeneo pekee. Kwa maana hiyo suala la mvua kuzuia shughuli za ujenzi sio changamoto kubwa sana kama jinsi inavyozungumziwa bali ni suala la kuangalia eneo husika na shughuli husika, kwa sababu sehemu kubwa sana ya shughuli za ujenzi hazizuiliwi na mvua wala msimu wa mvua haswa kama ilivyokuwa zamani.

Karibu sana

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *