NYUMBA NI UWEKEZAJI WA GHARAMA NA WA MUDA MREFU, FANYA MAAMUZI SAHIHI.

Kati ya kazi zinazolipa zaidi au zenye matokeo makubwa zaidi duniani ni kufanya maamuzi sahihi, kufanya maamuzi sahihi siku zote ndio sio kazi rahisi lakini ndio kazi inayopelekea matokeo bora sana. Kufanya maamuzi bora sio kitu rahisi lakini pia maamuzi bora yanafanywa na mtu mwenye kiwango cha juu cha uwezo na uelewa wa mambo mengi na hasa katika eneo analofanyia maamuzi. Hivyo mfanya maamuzi ili aweze kufanya maamuzi bora anapaswa kwanza awe ni mtu wa kusoma na kujifunza sana na pili anapaswa kuwa ni mtu mwenye uzoefu binafsi katika jambo hilo. Na hiyo ndio sababu wafanya maamuzi ni watu wakubwa na wenye maslahi makubwa sana. Kwa kifupi viongozi wote wa biashara na taasisi kazi ya kubwa ni kufanya maamuzi, mafanikio yao na mafaniko ya kampuni, biashara au taasisi husika yanayotokana na uwezo wao wa kufanya maamuzi bora.

Sasa kama jinsi tumeshaona hapo juu, ili mtu ufanye maamuzi bora unahitaji vitu vikubwa viwili, moja ni aidha uwe unasoma sana kuhusu kanuni mbalimbali za namna ya kuamua mambo kulingana na asili ya mambo yenye na namna yanavyoathiriwa na tabia za binadamu sambamba na kujifunza kupitia uzoefu binafsi na uzoefu waw engine na pili ni uwe na mshauri ambaye ana huo uwezo na uzoefu ambaye utakuwa unafanya maamuzi baada ya kumsikiliza yeye. Hata hivyo namba moja ndio sahihi zaidi kwa sababu licha ya mtu kuwa na mshauri bado sio mara zote atakubali kumsikiliza hasa ikiwa kuna maslahi yake binafsi anayahitaji kwa haraka hata kama mbeleni kuna matatizo kwa sababu binadamu tunaongozwa sana na hisia za tamaa na kupenda njia fupi. Hii ndio sababu watu wengi hufanya maamuzi yao binafsi kwa kutumia hisia na ndio maana wengi huishia kwenye majuto.

Kwenye masuala ya ujenzi napo mambo hayapo tofauti sana kwa sababu binadamu ni wale wale siku zote na sehemu kubwa ya maamuzi yao yanaongozwa na hisia. Hivyo utakuta watu wanafanya maamuzi muhimu ya mambo yatakayodumu kwa miaka mingi kuliko hata uhai wao hapa duniani lakini wanayafanya kwa namna rahisi sana. Kwa mfano utakuta mtu anatakiwa kupata mtaalamu aliyebobea kwa ajili ya kufanya kazi yake fulani ambayo inakwenda kumgharimu fedha nyingi sana na hata maisha yake kwa ujumla lakini mtu huyo unakuta anaogopa kutumia mtaalamu au anakimbia gharama za mtaalamu na kwenda kutafuta kanjanja au mtu wa bei rahisi ambaye hana uwezo mzuri katika mambo na kumpa kazi hiyo ambayo anaifanya wa viwango duni sana lakini gharama ya kuijenga inayokuja kutumika ni ile ile. Miradi hii tunakutana nayo kila siku tunapopita huko barabarani tunakutana nayo kila kona. Utakuta mtu anaenda kujenga jengo la milioni 100 lakini anatafuta mtaalamu atakayekamilisha kazi nzima ya kitaalamu ya jengo la milioni 100 kwa Tshs 100,000, hapa huhitaji kufikiria sana kujua kwamba huyu mtu anakwenda kutumia pesa nyingi kujenga nyumba ya viwango duni.

Sasa hayo ndio tunaita maamuzi mabovu, kwa sababu inahitaji tu kufikiria kwa makini kujua kwamba huwezi kufanya kazi nzima ya kitaalamu ambayo ndio inatoa mwongozo wote wa ujenzi kwa mradi wa Tshs milioni 100 kujaribu kukamilisha kazi ya kitaalamu kwa Tshs 100,000. Kwa watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri na wanaoelewa masuala ya usawa na ulinganyo wanaona kabisa kwamba mizania hii haijakaa sawa. Lakini sio kwamba hutapata mtu wa kufanya kazi hiyo kwa malipo yasiyoendana nayo, utampata lakini ni vigumu sana mtu huyo kufanya kazi bora hata kama itatokea kwamba mtu huyo ana ubora kwa sababu hata kanuni ya asili yenyewe inafanya kazi. Nikiongea kutoka kwenye uzoefu naweza kusema unajaribu kupata kitu cha ukweli(original) kwa bei ya kitu feki, hivyo utaishia kuuziwa kitu feki.

Kumbuka kwamba tofauti na nguo, viatu au hata simu, nyumba ni uwekezaji wa muda mrefu sana na wa gharama sana haipaswi mtu kuufanyia mizaha au kujaribu kuukamilisha kwa njia za mkato badala yake unapaswa kuupa hadhi na heshima inayostahili. Katika hili sasa ndipo watu wenye uwezo mkubwa kimaamuzi wanapoingia na ndio watu wa aina hiyo ambao hulipwa fedha nyingi sana au kufikisha taasisi, kampuni au biashara kwa viwango vya juu sana kwa maamuzi sahihi na bora wanayofanya yanayohusisha mtazamo mpana na kuangalia mbali.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *