NI MUHIMU KWA MSANIFU JENGO NA MHANDISI MIHIMILI WA JENGO KUELEWANA ILI LENGO NA NDOTO YA MTEJA VITIMIE.

Watu wengi ambao wako nje ya taaluma ya ujenzi huwa hawaelewi vizuri sana namna timu ya ujenzi inavyofanya kazi na mgawanyo wa majukumu yake katika kukamilisha utaratibu na mahitaji yote ya kitaalamu kuanzia katika hatua ya michoro ya jengo mpaka wakati wa ujenzi mpaka kukamilisha. Tofauti na watu walivyozoea kwamba jengo huwa na mhandisi ambaye amezoeleka zaidi kwa jina la “Engineer” ushauri wa kitaalamu wa jengo kwa hatua ya michoro mpaka ujenzi huhusisha mtaalamu zaidi ya mmoja, wanaweza kufika wataalamu wanne mpaka watano lakini wale ambao wanafanya kazi kubwa na inayochukua umakini mkubwa ni wawili ambao ni msanifu wa jengo(Architect) na mhandisi mihimili wa jengo(Structural Engineer).

Msanifu wa jengo(Architect) ndiye mbunifu mkuu wa jengo na ambaye huja na wazo jipya la mipangilio ya nafasi na mwonekano wa jengo ndani na nje ya jengo pamoja na mazingira yanayolizunguka jengo kisha mhandisi mihimili wa jengo(Structural Engineer) hufanya ubunifu wa mihimili inayohakikisha jengo ni imara na mzigo wote wa jengo unabebwa vizuri na mihimili inayolishikilia jengo. Msanifu wa jengo(Architect ) yeye huwepo kwenye kila aina ya jengo lakini mhandisi mihimili(Structural Engineer) wa jengo mara nyingi huwepo kwenye majengo ya ghorofa au yasiyo ya ghorofa lakini yanayohusisha mzigo mzito unaobebwa na jengo lenyewe. Msanifu wa jengo(Architect) baada ya kufanya ubunifu na kukamilisha kazi yake ndio humpa mhandisi mihimili(Structural Engineer) michoro hiyo naye afanye kazi ya kubuni na kufanya hesabu za kihandisi ili kupendekeza mfumo sahihi wa mihimili itakayomudu kubeba mzigo wa jengo husika.

Sasa ili kutimiza lengo na ndoto ya msanifu wa jengo sambamba na mteja wake kunahitajika kuwa na kuelewana kwa hali ya juu kati ya msanifu wa jengo na mhandisi mihimili wa jengo katika kutekeleza majukumo yao kwa mradi husika. Hii ni kwa sababu kuna wakati msanifu wa jengo anaweza kufanya kazi yake vizuri kisha akampa mhandisi wa jengo michoro yake ili naye afanye kazi yake kisha mhandisi wa jengo kutengeneza ramani za kihandisi ambazo zinaharibu au kupunguza ubora wa kazi ya kisanifu. Kwa mfano msanifu wa jengo anaweza kuwa amefanya kazi nzuri ya ukubwa wa mikutano au sherehe ambapo amefanya ubunifu mzuri wa eneo la ukumbi na mpangilio wa ukaaji wa watu kuelekea kwenye eneo la steji, kisha kumpa mhandisi mihimili ya jengo kufanya kazi ya ubunifu wa nguzo, boriti na sakafu kama mfumo mzima wa mihimili. Mhandisi mihimili anaweza kupendekeza mfumo ambao unaharibu ule mpangilio ambao mbunifu wa usanifu ameweka unaofanya kazi vizuri sana kwa yale matumizi yenyewe ya jengo yaliyokusudiwa.

Lakini ikiwa wataalamu hawa watakaa chini na kujadiliana kwa kina na kuelewana kwenye kila wanachofanya huku kila mmoja akijaribu kufikiria malengo na mipango ya mwingine kwa jengo husika basi wanaweza kufikia maamuzi bora ambayo yanaenda kutimiza matakwa ya taaluma zote mbili na kuongeza sana thamani ya jengo hilo. Karibu majengo yote huweza kuwa na changamoto hii ya kukosekana kwa maelewano baina ya taaluma hizi mbili na hususan majengo yenye maeneo makubwa kwa ndani kama vile kumbi za starehe na za mikutano, makanisa, misikiti n.k., Taaluma nyingine ambazo huingiliana pia na taaluma hizi ni pamoja na taaluma ya uhandisi huduma(sevice engineering) ambayo inahusisha uhandisi umene(electrical engineering), plumbing(bomba), mifumo ya computer, kiyoyozi n.k.,

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *