MSINGI MKUU WA MAFANIKIO KWENYE UJENZI NI UAMINIFU.

Kadiri ninavyoendelea kukua kuimarika kwenye tasnia hii ya ujenzi na ukandarasi wa miradi ya ujenzi kwa ujumla ndivyo ninavyozidi kuona jinsi suala la uaminifu ni changamoto kubwa lakini likiwa ndio eneo muhimu sana la mafanikio kwenye ujenzi. Lakini pia tasnia ya ujenzi imeendelea kunionyesha jinsi suala zima la uaminifu lilivyokuwa ni bidhaa hadimu sana kwa jamii ya binadamu. Dhana hii sio ngeni sana kwa sababu kitendo cha binadamu kuwa na hisia ya tamaa basi imekuwa kama ni laana kwake kwenye suala zima la uaminifu. Kitu cha kushangaza zaidi ni kwamba tamaa hii ipo kwenye maeneo yote kuanzia kwenye vitu vidogo mpaka kwenye vitu vikubwa kabisa.

Swali linakuja ni kwamba ni kwa nini sasa kwenye ukanda ujenzi kunakuwa na eneo maalum lenye taa nyingi nyekundu kwenye suala zima la uaminifu? Kwenye ukanda huu wa ujenzi suala la uaminifu ni changamoto zaidi kwa sababu kwanza kuna fursa kubwa na nyingi sana za watu kufanya udanganyifu ambao sio wa wazi lakini pia ukanda huu wa ujenzi unahusisha pesa nyingi sana ambazo zinawapa watu tamaa ya kukosa uaminifu hasa watu ambao bado hawana mafanikio makubwa kimaisha na hawana matumaini makubwa ya kufanya vizuri au kupata mafanikio kwenye maisha kwa kuwa waaminifu. Hili linapelekea watu kuamua kujiingiza kwenye hatari hizo za kukosa uaminifu kama njia ya mkato kwenye maisha kwani wanaamini wakiipoteza fursa kama hiyo itakuwa vigumu kuja kuipata tena huko mbeleni.

Hata hivyo pamoja na vishawishi vikubwa sana vya mtu kupata manufaa makubwa sana na ya muda mfupi kwa kukosa uaminifu kwenye ujenzi bado hakuna sehemu suala zima la uaminifu linalipa kwa kiasi kikubwa kama kwenye ukanda wa ujenzi. Mtu akiweza kujenga uaminifu kwenye kazi za ujenzi basi mtu huyo hujikuta akipata fursa nyingi za mafanikio kwani watu wa aina hiyo wanatafutwa sana kwenye ujenzi kwa udi na uvumba. Hata hivyo kuweza kufanikisha hilo mtu anapaswa kuwa ni wa kipekee sana kwani vishawishi vya kukosa uaminifu katika eneo ambalo wizi na udanganyifu una manufaa makubwa ya muda mfupi ni vikubwa sana.

Kwa upande wa mteja yeyote ambaye hajawahi kupitia changamoto ya kukutana na udanganyifu na wizi kwenye miradi ya ujenzi anapaswa kujua kwamba bado yeye ni mtu mwenye bahati sana kwani kukutana na uaminifu ni bahati ya kipekee. Lakini kwa yule ambaye ameshakutana na changamoto za kukosekana kwa uaminifu atakuwa anaijua vizuri thamani ya kufanya kazi na mtu mwaminifu na inamaana kubwa kiasi gani kwani kuibiwa kunauma na kuchukiza. Baadhi ya wateja ambao wameshaumia mara nyingi wanaamini kwamba huwezi kabisa kupata mtu mwaminifu wa kukufanyia kazi zako bali unapaswa tu kukuendelea kupambana mwenyewe na watu wasio waaminifu kwa njia zako mwenyewe. Ukweli ni kwamba watu waaminifu wapo lakini ni bahati sana kukutana nao.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *