NANI ANAKUWEPO KATIKA ENEO LA UJENZI MUDA WOTE?

Kumekuwepo na maswali mengi na sintofahamu kubwa juu ya uwepo wa wataalamu kwenye eneo la ujenzi wakati wote. Hili limekuwa likileta sana pia maswali kwa watu wengi ambao hawaelewi juu ya wasimamizi wa ujenzi ni nani na anayekuwepo katika eneo la ujenzi muda wote ni nani.

Kimsingi kabisa mtu ambaye unampata katika eneo la ujenzi muda wote ni msimamizi wa ujenzi ambaye amezoeleka kujulikana zaidi kama “Site Foreman”. Huyu ndiye mtu unayeweza kumpata wakati wote na ambaye ndiye anawajibika kwa watu wote wanaofanya kazi katika eneo la ujenzi sambamba na kuhakikisha taratibu zote na maelekezo yote yanafuatwa katika eneo la ujenzi. Watu wengine kama vile mtaalamu wa idara ya usanifu wa jengo na uhandisi mihimili wa jengo mara nyingi sio lazima umpate muda wote katika eneo la ujenzi. Kuna wakati wanakuwepo na kuna wakati hawapatikani kwani wao sio wasimamizi wa moja kwa moja wa taratibu zote na maelekezo yote yanayotolewa katika eneo la ujenzi japo ndio waamuzi wa mwisho kwenye idara hizo.

Jambo hili limekuwa likichanganya watu ambao hufikiri yule msimamizi wa ujenzi ambaye anapatikana muda wote katika eneo la ujenzi ndiye mhandisi mkuu wa kazi nzima ya ujenzi. Ukweli ni kwamba yule msimamizi anachofanya ni kuwawakilisha na kusimamia maamuzi na maagizo ya wataalamu wa ujenzi kuhakikisha yanatekelezwa kama yalivyoamuliwa. Hii ni sawa na watu wengine wowote wanapofanya maamuzi ya kufanya jambo na kutengeneza mpango mzima wa utekelezaji pamoja na kupeleka timu ya utekelezaji kwenye eneo la ujenzi kisha anakuwepo msimamizi wa kuhakikisha yote yaliyoamuliwa yanatekelezwa na kusimamia taratibu nyingine zote zilizopangwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kushughulikia dharura yoyote inayojitokeza kwa maelekezo kutoka kwa wataalamu husika.

Hata hivyo wataalamu husika au tunaweza kusema mhandisi/msanifu au injinia huwa wanapatikana pia mara kwa mara kadiri ya vile wanavyohitajika au wakati wa kila hatua muhimu ya kukagua na kuamua mambo yanayofanyika. Wataalamu hawa huwezi kuwapata muda wote hata ndani ya siku moja sio rahisi uwapate wakati wote kwa sababu akishapita katika eneo la ujenzi kuangalia kama mambo yote yako saw ana kujiridhisha huwa hawaoni sababu ya kuendelea kuwepo kwani utakuta ana majukumu mengine aidha ofisini au kwenye eneo jingine la ujenzi. Kutokwepo kwao hakuwezi kuharibu jambo ikiwa wanapita mara kwa mara na kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri na hivyo kinachoendelea ni utekelezaji tu wa mipango waliyoweka.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *