UNAHITAJI KUANZA MCHAKATO WA MRADI WAKO WA UJENZI SASA HIVI.

Watu wengi wana mtazamo kwamba watakuja kuanza kushughulika na miradi yao ya ujenzi wakati fulani muda ukifika. Labda wakishapata fedha au wakishanunua kiwanja/eneo wanalokwenda kujenga au labda wakishaanza mradi fulani ambao utakwenda kuwaletea pesa. Swali ni je, ni upi wakati sahihi kwako kuanza mradi wako wa ujenzi? Wakati sahihi wa kuanza mradi wako wa ujenzi ni sasa hivi, yaani leo au sasa hivi. Kuna umuhimu mkubwa na faida nyingi sana za kuanza safari ya mradi wako wa ujenzi sasa hivi au leo.

Kwa nini ni muhimu kuanza mchakato wa mradi wako wa ujenzi sasa hivi? Kwanza labda unasema bado hujanunua hata kiwanja. Ndio ni muhimu kuanza mchakato wa mradi wako wa ujenzi kabla hujanunua hata kiwanja kwa sababu zoezi la kununua kiwanja sahihi utaweza kulifanikisha kwa maamuzi sahihi ukiwa tayari una uelewa wa kile unachokwenda kujenga kuanzia ukubwa wa kiwanja chenyewe mpaka aina ya eneo ulilochagua kufanya ujenzi huo. Hii ni kwa sababu uzuri wa eneo ulilochagua unachangiwa na aina ya makazi au jengo unalokwenda kujenga hapo.

Kimsingi kabisa mtu unapaswa kuanza mchakato wa kuhusu mradi wa ujenzi wa nyumba yako katika hatua yoyote unayokuwepo na hatua ya kwanza kabisa unayopaswa kuchukua ni kuonana na mtaalamu wa ujenzi hususan wa kutoka katika tasnia ya usanifu majengo mkajadili mradi wako. Katika majadiliano hayo utagundua vitu vingi sana ambavyo ulikuwa hujui ambapo sasa kutokea hapo utaanza kuchukua hatua na kufanya maamuzi sahihi ambayo pengine usingefanya kama usingekutana na mshauri wa kitaalamu mkazungumza. Kuchukua hatua mapema kwa kuanza kukutana na mshauri wa kitaalamu utaweza kuepuka makosa mengi ambayo pia yatakuepushia upotevu wa fedha usiouhitaji.

Baada ya kujadili hayo na mtaalamu utajikuta unakwenda katika mamlaka mbalimbali kufuatilia vitu muhimu au kuulizia vitu ambavyo utapaswa kuvifahamu vizuri ili ufanye maamuzi sahihi ikiwemo gharama za vitu hivyo na michakato inayohitajika kuvikamilisha. Kwa maana hiyo kwa vyovyote vile unapaswa kuanza mchakato wa mradi wako wa ujenzi sasa hivi ili kupata uelewa sahihi na kuanza kuchukua hata kama bado huna kitu chochote kile kuanzia fedha mpaka eneo lenyewe la ujenzi. Hii ni kwa sababu kuna manufaa makubwa katika kufanya hivyo na utaepuka gharama nyingi na kuokoa muda mwingi amabo utaupoteza ikiwa utasubiri mpaka muda kamili wa kuanza kujenga ufike.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *