KAMA HUMUAMINI FUNDI WAKO NUNUA VIFAA VYA UJENZI MWENYEWE.

Uaminifu kwenye shughuli za ujenzi ni jambo lililoadimika sana. Hii ni kwa sababu wizi wa vifaa vya ujenzi unaonekana kuwa na faida kubwa sana kiasi cha watu kukubali kujiingiza kwenye hatari hiyo ya kushiriki vitendo hivyo vilivyokosa uadilifu. Mazingira ya kukabiliana na kuzuia wizi kwenye miradi ya ujenzi kwa miradi midogo bado ni jambo gumu sana hasa inapokuwa mteja hana mtu mwaminifu wa kumpa dhamani hiyo ya kununua vifaa vya ujenzi. Hivyo mtu unapokuwa huna imani na uadilifu wa mtu unayekwenda kumkabidhi mradi wako wa ujenzi ni vyema ukampa fedha ya ufundi peke yake tena kwa awamu baada ya kuwa amekamilisha hatua fulani kisha vifaa vya ujenzi ukanunua mwenyewe.

OLYMPUS DIGITAL CAMERA

Faida za kuamua kununua vifaa vya ujenzi peke yako pale unapodili na mtu asiyemwaminifu katika mradi wa ujenzi sio tu kwamba unaokoa gharama za vifaa ambayo ungeweza kuibiwa bali pia unahakikisha kwamba jengo lako linajengwa kwa viwango sahihi kwa kununua vifaa sahihi ambapo badala yake vingeweza kununuliwa feki kwa gharama ndogo ili fundi ajinufaishe mwenyewe. Hili la ununuzi wa vifaa feki kwa gharama rahisi limekuwa ni changamoto kubwa zaidi kwani ni rahisi mtu kufanya hivyo bila kugundulika kiurahisi kwa sababu idadi ya manunuzi inakuwa iko bayana, kisha baadaye baada ya mradi kuwa ulikwisha siku nyingi ndipo inagundulika wakati uharibifu ulishafanyika.

Hata hivyo suala la ununuzi wa vifaa vya ujenzi na usimamizi wake sio jambo rahisi sana kwa mtu wa kawaida asiye na uzoefu wa mambo ya ufundi kushughulika nalo kwani ni rahisi kupotoshwa na kufanya maamuzi yasiyo sahihi. Hivyo ni muhimu ikiwa mtu utatafuta mtu mwingine mwenye uzoefu ambaye pia atakuwa ni mshauri kwenye vifaa vya ujenzi huku wewe ukilipia moja kwa moja kwenye maduka ambao watasafirisha kupeleka kwenye eneo la ujenzi ambapo pia utaweka mlinzi wa kukagua na kusimamia uingiaji na utokaji wa vifaa hivyo vya ujenzi.

Lakini ikiwa yote hayo yanakuwa magumu kwako ni muhimu na vyema kutafuta watu waaminifu au kampuni ya uhakika utakayoingia nayo mkataba sahihi utakaokusaidia kupata kile unachotazamia kwa gharama mtakazokubaliana bila kuhofia kuibiwa au kufanyiwa kazi iliyo chini ya kiwango. Kampuni huwa na mifumo bora sana ya kuzuia wizi na ubadhirifu wa aina yoyote kwani zenyewe huingia mikataba na wateja ambapo kukitokea changamoto ya wizi kampuni yenyewe ndio inaumia na sio mteja.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *