KAZI BORA YA UJENZI NI ILE ILIYOTANGULIZA UTU KABLA YA MASLAHI.

Wote tunajua kwamba binadamu wengi kwa asili tuna asili ya ubinafsi na kuangalia kile tunachokipata katika jambo lolote tunaloamua kulifanya. Hakuna tatizo kwenye tabia hii ya asili kwa sababu kwanza ndio iliyosaidia dunia kufika hapa ilipofikia. Tatizo linakuja pale ambapo asili hii inakuwa ndio kitu pekee kinachomsukuma mtu bila kujali wala kujishughulisha na ubora wa ile huduma au bidhaa unayotoa kwa sababu hujali kabisa kuhusu watu na utu wao. Inachukua binadamu ambaye ni muungwana na mwenye kujali watu kuweza kuona kwamba licha ya kwamba kinachomsukuma yeye kuchukua hatua ya kutoa huduma kwa wengine ni yale maslahi anayopata lakini kwanza anapaswa kuweka mbele maslahi ya wengine kwa sababu anajali sana pia kuhusu utu wao.

Mtu anapoingia mkataba wa kujenga au kumfanyia mtu mradi wa ujenzi kwanza anapaswa kuelewa kwamba anakwenda kutumia sehemu kubwa sana ya kipato cha mteja wake katika mradi huo ambapo makosa au uzembe wa aina yoyote unakwenda kupelekea hasara kubwa kwa mteja husika. Hivyo mradi huo unatakiwa kuwekeza muda na umakini mkubwa na hata kudhibiti tamaa kwa kufanya kazi na watu wenye uwezo kuhakikisha kwamba kazi ya mteja wake ambayo amewekeza pesa nyingi unatendewa haki na mteja husika kuridhika. Hata hivyo mtu anayeweza kuona hilo ni mtu ambaye anajua thamani ya utu wa mtu na ile heshima aliyopewa kuwa ni bora kuliko tamaa zake binafsi ambazo hata hivyo zinakwenda kumwangamiza.

Watu wengi huwa wanashindwa kutunza uaminifu na kujiingiza kwenye tamaa zinazowapelekea kuharibu kazi za watu au kusababisha hasara kwa sababu wamekosa uungwana wa kutosha kujali kuhusu thamani ya mtu na utu wake. Ni watu wachache sana waliojaliwa karama hiyo ya uaminifu wa kuweka utu mbele na kujali zaidi kuhusu maslahi ya wateja wao na ubora wa kazi yao kwa ujumla na kupelekea kufanikisha kazi zao kwa viwango vya juu. Pale unapofanya kazi na mtu anayetambua thamani ya utu na heshima aliyopewa na kujua kwamba hivyo ni vitu vyenye thamani kubwa zaidi kuliko tamaa zilizomtawala basi una uhakika wa kufanya kazi bora ya ujenzi licha ya kwamba inahusisha fedha nyingi sana. Hivyo ni muhimu zaidi mtu unapotafuta watu wa kufanya nao kazi basi ukajaribu kuangalia watu wanaotambua thamani ya utu wa watu na wanaothamini ile heshima wanayopewa kiasi kwamba wanaweza kutawala tamaa zao zinazowapotosha na zitakazokwenda kuwaangamiza kabisa.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *