USAHIHI WA KAZI YA UJENZI NI ULE UNAOZINGATIA MUDA.

Katika hii dunia thamani ya vitu hupimwa kwa namna nyingi na ubora wa huduma pia ni moja ya thamani ya vitu ambavyo hupimwa kwa namna nyingi. Huduma za ukandarasi na ujenzi mbali na kupimwa kwa uwezo, vifaa na wataalamu pia hupimwa kwa unafuu na uharaka wa ukamilishaji wa mradi wa ujenzi kwenye eneo la muda. Wote tunajua kwamba muda wenyewe ni fedha na hivyo kuutumia vibaya ni kupoteza fedha. Katika kazi ya ujenzi kupoteza fedha kwa kushindwa kutumia muda vizuri husababisha hasara kwa pande mbili, kuanzia upande wa mjenzi au mkandarasi mpaka upande wa mteja na ndio maana upotezaji wa muda huhusishwa adhabu kwa miradi inayofuata taratibu.

Udhibiti wa kazi na muda kwenye mradi wa ujenzi ni moja kati ya ishara za kwamba mradi husika unafanyika kitaalamu na unakwenda kufikia malengo uliyowekewa na pande zote zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo. Mradi wa ujenzi usioziangatia muda ni mradi ambao unafanyika kiholela bila malengo na unapelekea hasara kwa pande zote zinazohusika na hata kuvunja taratibu za kisheria. Hata hivyo yapo mambo mbalimbali yanayoweza kusababisha mradi wa ujenzi kwenda nyuma ya muda licha ya kupangiliwa vizuri na kwa kufuata taratibu za kitaalamu.

Jambo kubwa ambalo mara nyingi huathiri muda ambao mradi umepangwa kukamilika huwa ni kukosekana kwa fedha. Kukosekana kwa fedha au rasilimali zinazohitajika katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi moja kwa moja hupelekea mradi wa ujenzi kujikuta uko nyuma ya muda uliopangwa. Mamlaka za udhibiti kwenye tasnia ya ujenzi kama vile bodi mbalimbali za kitaaluma na hata baadhi ya taasisi za serikali zinazohusika na masuala ya ujenzi huweza kusababisha mradi kuchelewa na kuwa nyuma ya muda uliopangwa kwa kuzuia mradi usiendelee au kusababisha misukosuko ambayo hupelekea mradi kwenda nje ya muda uliopangwa.

Hali ya hewa nayo ni moja ya sababu ambazo huwezi kusababisha mradi kwenda nje ya muda uliopangwa ambapo mara nyingi hili hutokea katika hatua za mwanzoni za mradi wa ujenzi. Kwenye hali ya hewa mara nyingi ni katika nyakati za mvua kubwa sana ambapo kuna baadhi ya kazi hulazimika kusimama kupisha mvua zikatike ambapo muda mwingi hupotea na kazi kushindwa kuendana na ratiba iliyopangwa na hivyo kwenda nje ya muda uliopangwa. Hii inaweza kuwa pamoja na majanga ya asili kama vile tetemeko la ardhi ambalo huweza kudhoofisha jengo au hata kubomoa kabisa mfano kimbunga kikali katika maeneo yenye vimbunga vikali.

Jambo la mwisho linaloweza kusababisha mradi kuchelewa ni uwezo mdogo wa mjenzi/mkandarasi au mipango duni ya mjenzi/mkandarasi katika utekelezaji wa mradi husika. Ikiwa mjenzi/mkandarasi hana timu yenye watu wenye uwezo wa kutosha kupanga na kujenga kwa ubora na kasi basi ni rahisi kujikuta mradi ukienda nje ya muda. Uzoefu  katika eneo hili unahusisha vitu vingi sana na sio tu uwezo wa kiufundi bali pia kuna mipango thabiti, upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kwa haraka na kwa kiasi kinachohitajika, kusimamia mafundi wafanye kiasi cha kazi kinachotakiwa na kwa ubora wa hali ya juu inachukua uwezo na uzoefu.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *