MSINGI WA JENGO
Msingi – Msingi wa jengo huhamisha uzito wa jengo kutoka kwenye jengo lenyewe kwenda ardhini. Msingi wa jengo huhakikisha jengo liko katika usawa sahihi na aina ya msingi wenyewe ndio huamua urefu au ukubwa wa jengo kwenda juu. Kila nguzo inayokuwepo katika jengo imejengewa msingi imara chini ambao ndio hupokea mzigo huo mzito na kuupeleka chini ardhini.
AINA KUU ZA MISNGI YA MAJENGO.
Kuna Aina Kuu Mbili Za Misingi Ya Majengo
- Misingi Ya Kina Kifupi
- Misingi Ya Kina Kirefu
-Misingi Ya Kina Kifupi – Misingi Ya Kina Kifupi ni ile misingi ya jengo inayokwenda kina kifupi cha wastani wa mita 1.5 chini ardhini.
-Misingi Ya Kina Kirefu – Misingi Ya Kina Kirefu ni ile misingi ya jengo inayokwenda kina kirefu sana cha wastani wa kati ya mita 20 mpaka mita 65 chini ardhini.
-Misingi ya kina kifupi hutumika kwa majengo madogo na mepesi wakati misingi ya kina kirefu hutumika kwa majengo makubwa na mazito.
1. AINA ZA MISINGI YA KINA KIFUPI
Kuna Aina Tatu Za Misingi Ya Kina Kifupi Ya Majengo
- Msingi Wa Nguzo Huru Zinazojitegemea(Individual footings foundation)
- Msingi Wa Nguzo Zilizounganishwa Zinazotegemeana(Strip footings foundation)
- Msingi Wa Sakafu Moja Kubwa(Mat or raft foundation)
-Msingi Wa Nguzo Huru Zinazojitegemea(Individual footing foundation), ndio msingi rahisi zaidi na ulizoelekea sana. Huu hutumika pale ambapo mzigo wa jengo unabebwa na nguzo. Hapa kila nguzo inakuwa na kitako chake kinachojitegemea.
-Msingi Wa Nguzo Zilizounganishwa Zinazotegemeana(Strip footings foundation), hii ni aina ya msingi ambao mzigo wa jengo hubebwa na nguzo pamoja na kuta, ambapo kunakuwa na muunganiko katika vitako vya nguzo vinavyounganishwa na zege lenye chuma ndani yake, kisha kuta zinajengwa juu yake ambazo ndio zinaungana na nguzo kubeba ule mzigo wa jengo badala ya kubebwa na nguzo moja moja peke yake.
-Msingi Wa Sakafu Moja Kubwa(Mat of Raft Foundation), mara nyingi aina hii ya msingi wa skafu moja kubwa unatumika pale inapotokea jengo linapoanzia chini ardhini(basement), yaani ghorofa inaanzia ndani ya ardhi. Katika msingi huu wa sakafu moja kubwa, lile eneo lote la jengo lililopo chini ardhini ndio linakuwa msingi wenyewe wa jengo, ambapo mzigo wote wa jengo unatawanywa kwenye sakafu nzima ya eneo la chini ardhini ya jengo. Pia aina hii ya msingi hutumika maeneo ambayo udongo sio imara vya kutosha kulihimili jengo hivyo mzigo wa jengo unabidi kutawanywa katika eneo kubwa.
2. MISINGI YA KINA KIREFU
Hii ni aina ya misingi ya jengo ambayo huenda chini sana ardhini kati ya mita 20 mpaka mita 65.
Misingi Ya Kina Kirefu Inatumika Katika Hali Zifuatazo
-Misingi ya kina kirefu inatumika pale inapotokea kwamba udogo wa juu wa eneo husika hauna uimara wa kutosha kubeba uzito wa jengo linalotaka kujengwa eneo husika, kwa hiyo inalazimu msingi wa jengo uende chini sana kufikia kuukuta udongo imara au mwamba uliopo chini ya ule udongo dhaifu wa juu.
-Msingi huu wa kina kirefu pia hutumika kama mzigo wa jengo ni mkubwa sana kiasi kwamba msingi wa kina kifupi hauwezi kuuhimili, kwa mfano majengo marefu sana kwenda juu angani.
AINA ZA MISINGI YA KINA KIREFU.
- Msingi Wa Kina Kirefu Unaofika Kwenye Mwamba Mgumu(End Bearing Pile)
- Msingi Wa Kina Kirefu Usiofika Kwenye Mwamba Mgumu(Friction Pile)
-Msingi Wa Kina Kirefu Unaofika Kwenye Mwamba Mgumu, ni aina ya msingi wa kina kirefu ambao unachimbwa mpaka kuukuta udongo imara au mwamba ambapo mzigo wa jengo utabebwa na mwamba mgumu kwa kupitia kusafirishwa na nguzo hizi ndefu, zinatoka juu zinaupita udongo dhaifu mpaka kufika kwenye udogo imara au mwamba.
-Msingi Wa Kina Kirefu Usiofika Kwenye Mwamba Mgumu, ni aina ya msingi wa kina kirefu ambapo nguzo za msingi huu zinazotoka juu lakini hazifiki kwenye udongo imara wala mwamba ila unahamishia mzigo wa jengo katika udongo kwa ule mkandamizo unaokutana nao chini ardhini na hasa ukizingatia kwamba hizi nguzo za msingi huu wa kina kirefu huwa za umbo la mviringo. Katika aina hii ya msingi wa kina kirefu huwa kadiri nguzo hizi zinavyokwenda chini zaidi ndivyo kadiri msingi huu unavyoweza kuhimili mzigo mkubwa zaidi.
Hata hivyo katika uhalisia na utekelezaji wa hii miradi majengo mengi huchanganya aina zote hizi mbili za msingi wa kina kirefu katika kuhimili mzigo wa jengo.
Na Architect Sebastian Moshi
+255717452790
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!