UBORA WA KAZI YA UJENZI HAUTOKEI KWA BAHATI MBAYA.
Ni sheria ya asili kwamba hakuna kitu kizuri na chenye ubora kinachoweza kutokea bila kuweka juhudi kubwa za makusudi na maarifa muhimu yaliyohusisha uzoefu wa hali juu katika kufanikisha jambo husika. Changamoto zinazojitokeza katika kila jambo bora linalofanyika ni nyingi sana na zinahitaji maarifa na kazi kubwa kukabiliana nazo na kupelekea matokeo bora yanayotarajiwa kutofikiwa kwa urahisi.
Katika ujenzi hakuna tofauti kwenye kupata matokeo bora, ili kufanikisha mradi wa ujenzi kwa viwango vya juu kunahitaji umakini wa hali ya juu kuanzia mwanzoni kabisa kabla ya kuanza kutengeneza ramani mpaka mwishoni kabisa kumalizia “finishing” na kukabidhi jengo.
Kwanza kabisa kabla ya ujenzi kuanza inatakiwa kukutana na mtaalamu wa ujenzi mwenye ujuzi na uzoefu mkubwa na kujadiliana naye kwa kina kuhusiana mradi husika, kujadili kila kipengele na njia bora zaidi ya kukikabili kisha baada ya kupata mwanga mkubwa juu ya njia bora na sahihi zaidi za kudili na mradi huo ndipo utaratibu wa kutengeneza ramani kwa ajili ya jengo/majengo husika unaanza. Zoezi lote hili linafanyika kwa umakini wa hali ya juu na kunawepo ushirikiano na kushirikishwa kwa pande zote juu ya kila kitu kinachofanyika na madhara yake ya mbele.
Baada ya kukamilisha mchakato wa kutengeneza ramani unafuata ujenzi ambao utahusisha usimamizi makini sana huku ratiba ya kinachoenda kufanyika ikiwa imeshatengenezwa na kueleweka vizuri kwa pande zote. Vikao vya mara kwa mara sana ni muhimu katika kuhakikisha kwamba kila kilichopangwa kinafanyika kwa usahihi na ubora wa kazi ni wa hali ya juu sana.
Kwa kufanya haya kazi ya ujenzi inaweza kuwa bora sana, lakini ni makosa makubwa kuanzisha mradi wa ujenzi bila kuweka umakini wa hali ya juu na kazi sambamba na vikao vya mara kwa mara vya mradi kisha kuwa na matumaini kwamba mradi utaenda vizuri na kuwa kwenye viwango bora, ni kujidanganya.
Architect Sebastian Moshi
Whatsapp/Call +255717452790
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!