MKANDARASI ANAPASWA AWE NA WASHAURI WA KITAALAMU ILI ASIHARIBU KAZI.
Kazi yoyote ili ifanyike kwa usahihi na kwa viwango vya juu inahitaji wataalamu waliobobea katika fani husika kushiriki na kutoa ushauri wa kitaalamu katika kufanikisha kwa viwango sahihi na vinavyotarajiwa kile ambacho kinafanyika. Hili ni suala linafanya kazi katika fani zote na katika kazi za miradi yote hasa miradi mikubwa.
Linapokuja suala la ujenzi mambo hayako tofauti kwani kunahitajika wataalamu wa fani za ujenzi wa usanifu majengo na uhandisi mihimili kuhusika katika kusimamia, kukagua na kudhibiti ubora katika miradi ya ujenzi.
Lakini miradi ya ujenzi mingi ya ukubwa wa kawaida hukabidhiwa kwa wakandarasi ambao wengi sio wa taaluma husika na mara nyingi utakuta ndio wenye maamuzi ya mwisho au ndio wanaoamua mwelekeo na ubora wa viwango vya mradi husika. Lakini kwa sababu hawana utaalamu au sio wabobezi wa taaluma husika maamuzi yao huwezi kuathiri ubora wa mradi au kusababisha uharibifu kabisa, hivyo kila mkandarasi ambaye sio mtaalamu wa fani yoyote ya ujenzi anapaswa kuwa na wataalamu wa fani hizo katika kila hatua wanayohusika.
Miradi mingi ya ujenzi mikubwa iliyoharibika au kufanyika chini ya viwango au hata kuharibu ile picha ya nje ya muonekano wa jengo husababishwa zaidi na ukandarasi ambao unashindwa kuzingatia aidha ushauri wa wataalamu au hakuna kabisa washauri wa kitaalamu katika mradi husika. Ukifanya ziara ya kutembelea maeneo mengi ya ujenzi utakuta mambo mengi yanaharibika kwa sababu mambo mengi yanafanyika bila kuzingatia utaalamu wa fani za ujenzi.
Architect Sebastian Moshi
Whatsapp/Call +255717452790.
Ninashukuru sana kwa maarifa haya mazuri,
Nakutakia kazi njema sana za uandishi.
Rafiki yako,
Aliko Musa.