FAHAMU CHANGAMOTO ZA MRADI WA UJENZI KUPITIA UZOEFU WA MIRADI MINGINE.

Wateja wengi wa miradi ya ujenzi huwa na mtazamo wa tofauti sana na uhalisia wa mambo ulivyo katika miradi ya ujenzi, na kwa baadhi imekuwa ni changamoto kuwashawishi juu ya umuhimu wa baadhi ya mambo yenye umuhimu katika mradi wa ujenzi. Imekuwa changamoto kuwashawishi juu ya umuhimu wa kuanza kutafuta mshauri wa kitaalamu akaandaa michoro ya ramani za ujenzi ambayo inaendana na mahitaji yake sambamba na hali halisi ya eneo lenyewe la ujenzi, imekuwa ni vigumu kumshawishi juu ya gharama halisi za ushauri wa kitaalamu, gharama halisi za vifaa na ufundi katika ujenzi. Imekuwa ni vigumu kuwashawishi juu ya muda na umuhimu wa ubora na umaridadi sambamba na gharama zake n.k

KUPATA UZOEFU WA MRADI AMBAO TAYARI UMESHAJENGWA UNASAIDIA KUPATA TAARIFA MUHIMU SANA ZENYE MSAADA MKUBWA KATIKA KUEPUKA MAKOSA

Sasa ili mtu kuondoa mashaka juu ya yale unayoambiwa na kufikiri pengine sio uhalisia na pia kuepuka wasio waaminifu ambao watakwepa kukuambia ukweli na uhalisia ili uwape kazi kisha waanze kukusumbua au hata kukimbia kabisa kwa sababu angalau wameshafanikisha kidogo walichokuwa wanalenga, ni vyema na muhimu sana ukatumia uzoefu wa watu wengine ambao wameshapitia zoezi kama hilo kujifunza na kuweza kuelewa uhalisia wa mambo ulivyo ili uweze kufanya maamuzi sahihi. Katika kutafuta uzoefu kwa watu ambao wameshapitia mchakato wa kujenga unapaswa kuwa makini na kwenda kimkakati ili uweze kuupata ukweli kwa sababu usipokuwa makini bado unaweza usipate taarifa sahihi sana na hivyo kujikuta ukifanya makosa tena, muhimu ni kuwa na akili ya kujiongeza ya namna ya kupata taarifa sahihi kutoka kwenye uzoefu wa mtu mwingine ambaye alishajenga mradi unaoendana na ambao unataka kujenga.

JAPO MIRADI YA UJENZI HAIWEZI KUFANANA KABISA LAKINI KUNA MENGI SANA YA KUJIFUNZA KUTOKA KWA MTU AMBAYE AMESHAPITA KATIKA UHALISIA

Kujifunza kupitia uzoefu wa wengine kutakusaidia kuondoa dhana na mitazamo ya kubashiri isiyo sahihi ndani ya akili yako na kuweza kuukabili uhalisia, jambo ambalo litakusaidia sana katika kufanya maamuzi sahihi na kuepuka majuto baadaye.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *