ONGEZEKO LA GHARAMA NDOGO NDOGO WAKATI WA UJENZI(VARIATIONS) NI MUHIMU.
Katika miradi ya ujenzi kuna kitu kitaalamu tunaita(variations), ambalo ni ongezeko la gharama ndogo ndogo za ujenzi wakati mradi ukiwa unaendelea. Ongezeko hili la gharama ndogo ndogo za ujenzi hutokana na sababu mbalimbali kwa mfano maamuzi mapya yaliyopelekea mabadiliko kiasi ambayo yanaathiri bajeti iliyokuwa imepangwa, mabadiliko ya hali ya hewa hususan mvua kubwa ambayo hayakutarajiwa na kusababisha baadhi ya kazi kusimama na kuathiri bajeti iliyokuwa imepangwa, maamuzi ya mamlaka za ujenzi ambayo yametoa amri kwamba yafanyike mabadiliko fulani ili kukidhi takwa fulani la kisheria lakini yanayoathiri bajeti iliyopangwa na au katika kurekebisha makosa yaliyosababishwa na kukosekana kwa taarifa sahihi katika muda sahihi na kuathiri bajeti iliyopangwa. Zote hizi na nyingine zaidi ni sababu zenye uhalali wa kuruhusu ongezeko la gharama ili kufanikisha mradi katika viwango vilivyopangwa vinavyotarajiwa.
Changamoto kubwa iliyopo kwenye miradi ya ujenzi na hasa miradi ya watu binafsi ni baadhi ya watu kuwa wagumu sana kuzitambua hizi “variations” ambazo hata katika hali ya kawaida kabisa zinaingia akilini na kutozitambua huku siku zote huwa kunakuja na gharama zake. Lakini kwa upande mwingine pia upande wa wajenzi nao wanaweza aidha kuogopa au kushindwa kuzielezea kwa usahihi gharama hizi na hivyo kujikuta mradi ukipitia kwenye changamoto na hivyo kufanyika chini ya viwango. Jambo ni muhimu la kuzingatia wewe kama mteja ni kwamba ni mara chache sana mjenzi akakubali kutoa fedha zake kama sehemu ya faida kugharamia kazi ambayo anaamini ni jukumu la mteja na hivyo anachofanya ni kufanya kazi hiyo chini ya kiwango au kuchakachua sehemu nyingine ili kufidia eneo hilo aweze kumaliza kazi hiyo bila kujali amefanya kwa kiwango gani. Hivyo ni muhimu na busara kwa mteja kujitahidi kuhakikisha kwamba kazi husika inafanyika kwa viwango sahihi kwa kukaa chini na kuzungumza na mjenzi/mkandarasi namna watahakikisha hilo linafanikiwa na mara nyingi ni kwa mteja kukushiriki gharama hiyo hata kama haitakuwa kwa asilimia 100% ili mwisho wa siku kazi isije kufanyika kwa viwango duni kwa sababu tu ya ubishi kwenye kiasi kidogo cha pesa ukilinganisha na thamani ya mradi wote ambayo ni kubwa sana.
Ongezeko la gharama ndogo ndogo za ujenzi “variations” wakati wa ujenzi ni jambo linalojulikana kisheria katika miradi ya ujenzi pengine hata kwenye miradi mingine pia katika sekta nyingine.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!