UTARATIBU MZURI WA MALIPO YA USHAURI WA KITAALAMU KATIKA HATUA YA MICHORO YA RAMANI
Utaratibu wa namna malipo ya kazi ya ushauri wa kitaalamu katika hatua ya michoro ya ramani yanavyofanyika inaweza kuwa na madhara mbalimbali katika utekelezaji wa kazi hiyo. Kwanza kabisa kazi inayoanza kabla ya kiasi chochote cha pesa kulipwa mara nyingi huchelewa kufanyika kwa sababu huonekana haina haraka wala umuhimu na mtaaalamu pia hukosa uhakika wa kama mradi husika uko “serious” au bado hauna haraka wala umuhimu kitu ambacho hupelekea mradi kuchelewa kwa kutopewa umuhimu. Lakini pia kama pesa yote ikilipwa mwanzoni kwa mara moja huweza kuwa na madhara kwa aliyelipwa kwa kuwa ameshalipwa hela yote anaweza kukosa msukumo wa kufanya kazi kwa haraka kwa sababu kile kinachompa msukumo ambacho ni pesa ameshachukua chote na hakuna kitu cha ziada anachotegemea hivyo utaratibu wa kulipa yote inatakiwa ukutane na mtu mwenye nidhamu binafsi ya kazi au kampuni yenye utaratibu makini sana katika utekelezaji.
Kwa hiyo njia nzuri ya kufanya utaratibu wa malipo ya gharama hizi ni kufanya malipo kwa namna itakayojenga hamasa, msukumo na kuhakikisha ubora wa kazi unazingatiwa. Kwa maana hiyo malipo haya yanapaswa kugawanywa mara tatu au endapo tatu itaonekana ni usumbufu sana basi angalau mara mbili. Nashauri mara tatu kwa sababu ili upate kazi nzuri itakuhitaji kufuatilia viwango vya namna kazi husika inafanyika ambapo baada ya kujiridhisha na ubora wa mtaalamu husika katika huduma za ushauri wa kitaalamu na mkawa mmeshakubaliana kila kitu juu ya nini haswa kinakwenda kufanyika basi inabidi umlipa angalau asilimia 30% ya gharama ya kiasi mlichokubaliana. Yaani kwa mfano mmekubaliana gharama ya kazi nzima ni Tshs 1,000,000 basi inabidi umlipe malipo ya awali ya angalau Tshs 300,000. Kisha atafanya kazi ya kuja na wazo na mpangilio wa kila kitu katika jengo hilo na kuonyesha utaratibu mzima wa namna jengo husika linafanya kazi na namna huduma zote ndani ya jengo zinafanya kazi, ambapo sasa wewe utatoa maoni yako kutokana na maelezo yake na ikiwa unahitaji marekebisho kadha wa kadha yatatakiwa kufanyika kadiri ya mlivyokubaliana. Hapa wewe mwenyewe unaweza hata kama ni kumwonyesha mtu wako wa karibu au familia yako ikiwa unahitaji ushauri zaidi au nyongeza yoyote ya kile ambacho mnafikiri ni muhimu au mnakihitaji.
Baada ya hatua hiyo na kujiridhisha na kazi yako sasa utamlipa kiasi kingine cha asilimia 40% ya kazi yote ya ujenzi yaani Tshs 400,000 katika kile kiasi cha Tshs 1,000,000 mlichokubaliana na sasa ataenda kufanya kazi ya kutengeneza mwonekano wa jengo pamoja na vipengele vyote muhimu vya jengo vinavyoongeza ubora wa kimuonekano na kuvutia pamoja na mengine ambayo yana umuhimu kama vizuizi vya juu, ukubwa wa milango na madirisha utaonekana n.k., na baada ya hapo atakuja mtajadili na kukubaliana baada ya kuafikiana kwenye kila kipengele na kazi husika. Baada ya kuafikiana kwenye hatua hii mtaalamu husika ataenda kufanya michoro ya mwisho yenye vipimo vyote tayari kwa ajili ya ujenzi na kama unahitaji kufuatilia kibali cha ujenzi basi atatakiwa kuhakikisha kwamba michoro hiyo imekidhi vigezo na masharti yaliyowekwa na mamlaka husika, na baada ya kukabidhi michoro hiyo ya mwisho iliyozingatia vigezo vyote na taratibu zote zinazotakiwa ndio utamalizia kiasi cha mwisho cha fedha zilizobaki ambayo ni asilimia 30% ya mwisho kwa maana ya ile Tshs 300,000 iliyobaki katika ile Tshs 1,000,000 mliyokubaliana.
Unapofuata utaratibu mzuri wa malipo kama huu ambapo muhimu pia ni kuwekeana tarehe ya mwisho ya kuwa hatua fulani imemalizika, basi unakuwa kwenye nafasi nzuri sana kupata kazi iliyo bora na uliyoiridhia ambayo pia imefanyika kwa muda uliopangwa na kuzingatia mambo yote muhimu ya pande zote mbili.
Architect Sebastian Moshi
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!