MIUNDO MBALIMBALI YA KISANIFU YA NYUMBA NA MAJENGO INA MAANA NA UMUHIMU FULANI KIHISTORIA.
Miundo mbalimbali inayoleta muonekano wa tofauti ikiwa ni mjumuisho wa vipengele vingi sana katika nyumba na majengo imekuwa mingi na ya aina tofauti tofauti na kila moja ikivutia watu tofauti tofauti huku mingine ikiwa na umaarufu mkubwa na mingine kuwa ya kawaida. Miundo hii imekuwa ni sehemu muhimu sana ya majengo tangu kale kabisa miaka zaidi ya 12,000 iliyopita wakati mawazo mbalimbali ya namna ya kubuni mionekano ya majengo inazaliwa. Miundo hii imekuwa ikachangiwa na tamaduni, mila, desturi, imani za kidini, mazingira, historia, hali ya hewa ya mahali ilipoanzia, mifumo ya utawala, umuhimu kijeshi, ufahari n.k.,. Miundo hii imekuwa ikiendelea kuboreshwa au kubadilishwa na namna mbalimbali na wakati mwingine kuchanganywa changanywa na kuzalisha aina nyingi za tofauti na zenye mionekano ya namna ya tofauti.
Hivyo staili na aina nyingi ya majengo mengi unayoyaona leo ni mjumuisho na mwendelezo wa staili nyingi zilizopita miaka mingi inayotokana na muingiliano tamaduni mbalimbali zinazojenga tamaduni mpya na mazoea mapya kutoka kwenye tamaduni zilizopita. Kumekuwepo kuiga, kuboresha na kuendeleza staili mbalimbali kwa maelfu ya miaka mpaka sasa. Kwa mfano uwepo wa baraza ya mbele ya nyumba ambayo ina nafasi ya kutosha na umuhimu mkubwa na ambayo imepambwa vizuri na inayoboresha muonekano wa mbele wa jengo na kulifanya livutie zaidi ni utamaduni ulioanzia Uyunani ya kale miaka takriban 2,500 iliyopita. Katika Misri ya kale ambapo staili mbalimbali za majengo zilikuwa na umuhimu tangu takriban zaidi ya miaka 5,000 iliyopita kipengele hiki cha kuboresha sana eneo la mbele kwa kuboresha baraza ya mbele hakikupewa umuhimu mkubwa kama kilivyokuja kupewa kwenye majengo ya Uyunani ya kale ambayo nayo kwa sehemu kubwa kuna vipengele yaliiga na kuboresha zaidi kutoka kwenye usanifu wa Misri ya kale. Mahekali mbalimbali na baadaye makanisa na misikiti yalijengwa kutokana na tamaduni na umuhimu wa kiimani wa miundo husika inayojumuishwa na vipengele vilivyowekwa vinavyoleta maana fulani kihistoria. Hata hivyo kuna vipengele vingine katika majengo ambavyo vinawekwa kwa ajili ya kuongeza uzuri wa muonekano na mvuto na sio lazima kuwa na umhimu wa kitamaduni, kihistoria au kiimani kuanzia chini kabisa kwenye jengo, mpaka muundo wa upauaji.
Tunapokuwa tunafanya kazi za kisanifu wakati mwingine tunaweza kuongeza ubunifu wa namna yoyote, iwe ni wa kimvuto au ni wa kitamaduni unaoweza kuvutia wengi na kupata umaarufu na pale wengi watapoiga na kuboresha inaweza kuwa ni staili mpya inayoweza kuingia kwenye historia na kuwa sehemu ya historia kubwa na kongwe ya miundo mbalimbali ya kisanifu.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!