Anza na Ramani

Unapoanza kufikiria kuhusu kujenga baada ya kuwa umepata ardhi kitu cha kwanza unatakiwa kufikiria ni ramani, na sio ramani ya kuungaunga bali unatakiwa kumtafuta mtaalamu kabisa ukae naye chini mjadili kwa marefu na kwa usahihi kuhusu kile unacholenga na namna kinaenda kutekelezwa. Hivyo kitu cha kwanza cha muhimu kabisa kuanza nacho ni ramani kwa sababu.

– Ramani ndio itakayokupa mwongozo wa kila kitu kinachoenda kufanyika, kuanzia vipimo, mpangilio, mwonekano mpaka uelekeo sahihi wa jingo, hivyo hilo linapaswa kuwa ndio kipaumbele cha kwanza.

Ramani Ya Nyumba Inatoa Mwongozo wa Jengo Linavyopaswa Kuonekana

– Ramani itakuhakikishia kupata matokeo uliyoyakusudia kwani utakakuwa tayari una kila kitu katika michoro na picha kabla haijaanza kujengwa na hivyo utahakikisha kila kitu kinafanyika kama ilivyofanyika katika michoro.

– Ramani itakusaidia kupata kile hasa unachokitaka na kukipenda na hivyo utaweza kuifurahia nyumba yako maisha yako yote utakayokuwa ukiiangalia kwani inakuwa imefanyika vile hasa inavyokuvutia.

Muonekano wa Ramani Ya Nyumba Kwa Nje

– Ramani itakusaidia kupata mpangilio sahihi ndani ya nyumba ambao utaendana mambo unayotaka kuanzia faragha za vyooni na bafuni, ustaarabu unaoletwa na mpangilio wa vyumba mahusiano yake na kingine, eneo na ukubwa wa jiko na baraza yake n.k., ambapo vitu hivi vitakufanya uishi kwa utulivu mkubwa na Amani ndani ya nyumba yako.

-Ramani itakuongezea ari, shauku na msukumo wa kujenga nyumba yako kwani utakavyoiona utatamani zaidi uikamilisha kwani utakuwa umeona haswa matokeo unayoenda kuyapata, hili litakufanya uwahi kukamilisha nyumba yako haraka zaidi ya vile ungekuwa huna ramani.

Ramani Ya Nyumba Inakuongezea Shauku Ya Kutamani Kuikamilisha

– Ramani inakusaidia kujua gharama sahihi za kila kitu mwanzoni kabisa kwani unakuwa tayati unacho unachokwenda kukifanyia kazi, kujua gharama kutakupa picha halisi na kukusaidia kujipanga na kupanga vizuri awamu za ujenzi wako, kwa sababu ukubwa wa ramani ndio unaoamua gharama za ujenzi.

– Ramani itakusaidia kuepuka kuchakachuliwa kwa jingo na watu unaowapa kazi ya kujenga kwa huwa inatokea wanaojenga wanaamua kupunguza baadhi ya vitu au ukubwa wa vyumba ili kuongeza faida au na kupunguza vifaa na ufundi, lakini ramani itawazuia kwani utakuwa unahakikisha vipimo sahihi vya kwenye ramani ndivo vilivyofuatwa.

Ramani Husika Inaepusha Uchakachuaji

– Ramani itakuweka kwa nafasi nzuri ya kuepuka kusumbuliwa na mamlaka husika kwa sababu mtaalamu wa kuchora ramani atazingatia taratibu zote za kimamlaka na kufuata vipimo sahihi vya umbali kutoka kwenye mipaka uliowekwa na mamlaka husika, pia ukiw ana ramani ni rahisi kuitumia kushawishi mamlaka husika kwamba ulifuata taratibu maalumu kabla ya kujenga hivyo kuepuka kuvunjiwa nyumba au kuvunjiwa sehemu ya nyumba.

– Ramani itakusaidia kuepuka kuja kujutia baadaye juu ya makosa mengi yatakayokuwepo ndani ya nyumba mara baada ya kuanza kutumia jengo hilo na kuanza kukutana na uhalisia ambao hukuufahamu mwanzoni na kubadilisha inakuwa aidha haiwezekani au inaambatana na gharama kubwa sana.

Ramani Ya Nyumba Inaepusha Majuto Ya Baadaye

– Ramani itakurahisishia kukubalika na taasisi za kifedha pale utakapotaka aidha kuchukua mkopo au kuikatia nyumba bima au kuifanya tathmini ya thamani nyumba kwa sababu zozote zile.

– Ramani itakusaidia ikiwa utahitaji kufanya mabadiliko ya jengo ili kubadili matumizi au kuongeza idiadi ya vyumba ua kubadili matumizi ya baadhi ya vyumba ambapo utaepuka kuanza kuchora upya na badala yale utatumia ramani iliyopo kufanya hayo marekebisho kwa kuirekebisha kiasi.

Ramani Ya Nyumba/Jengo Inarahisisha Kubadili Matumizi Ya Jengo au Vyumba Ndani Ya Jengo Kwa Baadaye

– Ramani inakupa nafasi ya kuhakikisha kila chumba kinapata ukubwa halisi unaouhitaji kadiri ya mahitaji yako kwa kuzingatia vile ulivyozoea kwenye nyumba uliokuwa unaishi kabla hujajenga ya kwako.

– Ramani itakusaidia kujua uwiano kati ya ukubwa wa kiwanja chako na nyumba unayotaka kujenga hivyo kuweza kujua ni eneo kubwa kiasi gani linalobakia kwa ajili ya matumizi mengine hapo nyumbani kwako kama vile parking ya magari, bustani, ufugaji, servant quarter, swimming pool na eneo la wazi.

Ramani Ya Nyumba/Jengo Itakupa Uelekeo na Uwiano wa Matumizi Sahihi Ya Kiwanja

Gharama ya ramani ni kidogo sana ukilinganisha na gharama unazokwenda kutumia kwenye nyumba unayojenga, hivyo itakuwa ni maamuzi yasiyo sahihi kabisa kutoweka uzito kwenye ramani ukifikiri unapunguza gharama wakati ramani ndiyo muhimu zaidi pengine kuliko hata baadhi ya hatua za ujenzi ambazo utagharamia pesa nyingi kuliko ramani. Gharama ya ramani mara nyingi inachukua chini asilimia 2% ya gharama za ujenzi wote.

Anza na ramani kuokoa gharama na ubora wa nyumba/jengo lako, kukwepa ramani au kuokoteza okoteza ramani ni hasara kubwa zaidi kuliko kufanya ramani yenyewe.

Kukwepa Ramani Ni Kubwa Kubwa, Kuokoteza Okoteza Ramani Ni Hasara Kubwa

Ahsante sana.

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *