UJENZI BORA AU BEI NDOGO?

Kwa kawaida maamuzi tunayofanya hutokana na hisia zilizojengeka ndani yetu kwa namna tulivyozoea mambo au vile tumekuwa tukiona mambo yakifanyika katika mazingira tuliyokulia. Hali hii imekuwa na changamoto sana kwani namna hii ya kufanya maamuzi kwa hisia na mazoea kumepelekea wengi kufanya maamuzi mabovu ambayo yamekuja kuwagharimu baadaye na kuwa majuto.

Linapokuja suala linalohusisha pesa hasa pesa nyingi, wengi wetu kutokana na malezi na hofu tulizopandikizwa tangu utotoni na aina ya maisha tuliyokulia tumekuwa moja kwa moja tunakimbilia kwenye bei rahisi bila kufikiria kabisa ubora au thamani ya huduma au bidhaa kwa uwiano na bei husika. Busara na akili ni kuangalia thamani na ubora kwanza kulinganisha na bei badala ya kukimbilia kwenye bei peke yake na hili ni kuanzia kwenye vifaa mpaka kwenye ufundi.

Miradi ya ujenzi nayo kama kitu kinachohusisha pesa nyingi imekuwa sehemu ya mkumbo huu wa watu kukimbilia kuangalia bei ndogo badala ya kuangalia ubora wa ujenzi, jambo ambalo limeleta hasara na majuto mengi baadaye kutokana na gharama zinazohusikana na ujenzi hivyo kama ni uharibifu umefanyika unakuwa unahusisha gharama nyingine kubwa kufanya marekebisho.

Miradi Ya Ujenzi Ina Gharama Kubwa

Zifuataza ni Changamoto zinazosababishwa na kukimbilia kwenye bei ndogo kabla ya kufikiria kuhusu ubora wa ujenzi wenyewe.

  • Ujenzi ni uwekezaji wa muda mrefu, ni kitu kinachotegemewa kudumu kwa wastani wa miaka sio pungufu ya 100 hivyo mtu unapofanya maamuzi ni vyema na muhimu kufikiria hili na kuona ni kiasi gani unahitaji kufanya ubora kuwa kipaumbele chako cha kwanza kabla ya kukimbilia kwenye beo ndogo. Ujenzi bora unazingatia uimara na usahihi wa utaalamu husika ambao unahusisha watu wenye uwezo na uzoefu na ambao wako kwa ajili ya kutoa huduma bora na sahihi.
Ujenzi Bora Unazingatia Uimara na Usahihi wa Utalaamu
  • Kukimbilia kwenye bei ndogo mara nyingi hupelekea kuja kuingia kwenye gharama kubwa zaidi hata kuzidi ambazo ungetumia mwanzo katika ujenzi bora. Hili linatokea kila siku na binafsi nimekutana nalo mara kadhaa pale mteja anapokuwa hana uelewa sahihi wa mambo ya ujenzi na hivyo kwenye kufanya maamuzi anaangalia bei ndogo peke yake bila kujihangaisha na ubora wa huduma za ujenzi.
  • Kukimbilia kwenye bei ndogo bila kuangalia ubora wa ujenzi husika mara nyingi hupelekea makosa madogo madogo na uharibifu ambao huja kukukasirisha sana baadaye pale unapoanza kuitumia nyumba.
Ujenzi Dhaifu Husababisha Makosa Madogo Madogo Ambayo Huja Kukukasirisha Sana Baadaye
  • Kitu kingine cha ajabu na kinachoshangaza zaidi kuhusu watu na tabia ya kukimbilia kwenye bei ndogo ni pale unapokuta mtu yupo tayari kutumia pesa nyingi sana kwenye kununua vifaa na malighafi za ujenzi kwa gharama kubwa lakini hayupo tayari kutafuta mtu mwenye uwezo wa kutosha kutumia vifaa hivyo na malighafi hizo kwa usahihi. Hivyo anatumia pesa nyingi kununua vifaa ambavyo vinajengwa hovyo hovyo na kukosa ubora kwa sababu ya kukimbilia beo ndogo. Kama uko tayari kutumia milioni 100 hupaswi kuona ni tatizo kutumia milioni 35 kuhakikisha vifaa ulivyonunua vinakuletea kitu chenye ubora utakachojivunia maisha yako yote badala ya kulazimisha kutumia milioni 20 ambayo utakuja kuishia kujilaumu mwenyewe na kulaumu wengine pia kwa maamuzi yako mwenyewe.
  • Ujenzi unapokuwa katika viwango duni utaonekana wazi na kupelekea aibu na kuonekana mzembe kitu kitakachokuumiza sana kwani utakuwa tayari umetumia pesa nyingi katika kununua vifaa lakini bado watu wanakuchukulia kama mtu mzembe na asiyeweza kufanya maamuzi sahihi.
Kazi Ya Ujenzi Ikiharibika Haifichiki Fanya Maamuzi Sahihi Kuepuka Kuonakena Mzembe
  • Kukimbilia kwenye bei ndogo mara nyingi huleta majuto ya baadaye ambayo utaenda nayo kwa muda mrefu sana kwani utaendelea kuiona nyumba/jengo lako wakati wote.
  • Hisia za kukimbilia kwenye bei ndogo ni za muda tu kwani baadaye utakuja kugundua hakuna kikubwa ulichokuwa unakwepa na ulichokataa hakina maana kubwa sana ukilinganisha na gharama kubwa au hasara utkayoingia.
Kung’ang’ania Bei Ndogo Ni Hisia Za Muda Tu, Baadaye Utakuja Kugundua Ulifanya Makosa.

Fanya maamuzi sahihi na ya busara, hakikisha kipaumbele chako namba moja ni kuangalia ubora na thamani ya huduma ya ujenzi unayokwenda kupata kabla hujakimbilia kwenye bei ndogo na baadaye utafurahia maamuzi yako mwenyewe.

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790

1 reply
  1. francis lauwo
    francis lauwo says:

    appreciate.changamoto za kitu unachoongelea ndizo changamoto nazoziona sasa hivi kwa injinia ambaye niko naye. mimi ni msimamizi tu katika kazi zake ila kwa kweli yuko nyuma sana kwenye kuplan na kuorganize kazi zake,kubudget,kwenye bei na mafundi(analalia na kutafuta mafundo wenye bei nafuu,ambao hawana utaalam),na yote katika yote ubora wa kazi zake..very poor.

    Reply

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *