TAARIFA MUHIMU ZA “SIATI” ANAZOPASWA KUZIFAHAMU MTAALAMU WA UJENZI KABLA YA KUTENGENEZA RAMANI.

Ili mtaalamu wa ujenzi awe katika nafasi sahihi ya kutengeneza ramani ya ujenzi inayoendana na eneo husika la ujenzi na iliyozingatia vigezo vyote muhimu kuna taarifa kadhaa muhimu anapaswa kuzifahamu hasa kama hajafika eneo lenyewe husika.

MTAALAMU WA UJENZI ANAPASWA KUWA NA TAARIFA ZOTE MUHIMU ZA ENEO LA UJENZI KABLA YA KUANDAA RAMANI

Kwanza kabisa mtaalamu wa ujenzi anapaswa kufahamu ukubwa wa kiwanja na vipimo vyake vyote vya pande zote za kiwanja kadiri ya umbo la kiwanja husika. Mtaalamu wa ujenzi anapaswa kufahamu hali ya kiwanja kwa maana ya uwepo wa kitu chochote katika eneo la ujenzi kama vile jengo lingine, gofu, mwinuko mkali au mteremko, mto au mfereji n.k.,. Mtaalamu wa ujenzi pia anapaswa kufahamu hadhi ya kiwanja kwa maana ya ikiwa kiwanja hicho kimepimwa au bado hakijapimwa na kama kimepimwa ikiwa nyaraka rasmi za taarifa hizo zilizopitishwa na mamlaka husika zimeshatoka. Mtaalamu wa ujenzi anapaswa kufahamu hali ya ardhi na udongo wa sehemu husika kama ikiwa ni udongo wa mchanga, mfinyanzi, tifutifu au aina nyingine yoyote pia anapaswa kujua kama eneo husika lina mawe makubwa au miamba na ukubwa wake ikiwa ardhi ya eneo husika iko hivyo.

MTAALAMU WA UJENZI ANAPASWA KUJUA HADHI YA KIWANJA NA HADHI YA MJI KILIPO KIWANJA HUSIKA

Mtaalamu wa ujenzi kabla ya kutengeneza ramani anapaswa pia kufahamu ikiwa eneo husika ni karibu na mlima mkubwa au bahari, basi mtaalamu wa ujenzi anapaswa kujua uelekeo wa ilipo bahari au mlima huo mkubwa kutokea kilipo kiwanja. Mtaalmu wa ujenzi anapaswa kujua eneo ambako zinapita barabara karibu au zilizopakana na eneo linalojengwa pamoja na hali ya viwanja vingine vinavyozunguka kiwanja husika na ikiwa vimejengwa au la, na hata aina na ukubwa wa majengo hayo ikiwa viwanja hivyo vimejengwa. Mtaalamu wa ujenzi atapaswa kujua kama eneo hili linalojengwa ikiwa ni eneo la mjini au kijijini au ni mji mdogo au mkubwa. Kwa taarifa hizo hapo juu mtaalamu wa ujenzi anakuwa kwenye nafasi sahihi sana ya kutengeneza ramani nzuri na yenye vigezo vyote muhimu vinavyoendana uhalisi wa eneo husika wa linapojengwa jengo hilo.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *