MZUNGUKO WA HEWA NDANI YA CHUMBA (CROSS VENTILATION).

Katika taaluma ya usanifu majengo kuna dhana moja inaitwa “cross ventilation” au mzunguko wa hewa ndani ya chumba. Hii ni ile hali ya kwamba chumba kinakuwa na uwazi zaidi ya mmoja kwa maana ya dirisha au venti ambapo hewa inaingilia kwenye dirisha moja na kutoka kwenye dirisha jingine au venti jambo ambalo linasaidia wakati wote chumba kuwa na hewa safi na laini kwa sababu hewa inaingia na kutoka muda wote. Kwa chumba ambacho kina uwazi mmoja pekee kama vile dirisha moja mzunguko wa hewa sio mkubwa sana kwa sababu hewa inaingilia na kutokea sehemu moja hivyo hewa inakuwa nzito kidogo japo sio sana ukilinganisha na chumba chenye uwazi zaidi ya mmoja au chenye uwazi mmoja mkubwa sana.

MZUNGUKO WA HEWA NDANI YA CHUMBA UNAWEZESHWA NA KUWEPO NA UWAZI ZAIDI YA MMOJA KWENYE CHUMBA

Sasa tunapokuja kwenye suala la vyumba ndani ya nyumba tunaweza kuona ni jambo zuri na muhimu sana chumba kuwa na uwazi zaidi ya mmoja kwa ajili ya kuingiza na kutoa hewa ndani ya chumba. Lakini kwa sababu ya changamoto mbalimbali za kisanifu na hasa kwa majengo makubwa au nyumba ya kuishi yenye vyumba vingi utakuta kuna wakati suala la kuweka uwazi zaidi ya mmoja kwenye chumba linakuwa changamoto kubwa sana ambapo mara nyingi watu huacha uwazi mmoja ambao unatosha kabisa lakini hewa ndani ya chumba inakuwa nzito kiasi ukilinganisha na chumba chenye uwazi zaidi ya mmoja. Kutokana na changamoto hii ya wingi wa vyumba na ukubwa wa nyumba unaosababisha chumba kushindwa kupata pande mbili zinazotazama nje hivyo kulazimika kutumia upande mmoja pekee kuweka dirisha au uwazi mwingine wowote basi hapa mtaalamu anaweza kutumia upande huo huo mmoja kuweka dirisha moja na venti juu au madirisha mawili kama ni upande mrefu vya kutosha.

CHUMBA KINAPOKUWA NA UWAZI ZAIDI YA MMOJA INARAHISISHA SANA MZUNGUKO WA HEWA NA KUONDOA HEWA NZITO NDANI YA CHUMBA

Mzunguko wa hawa ndani ya chumba unasaidia sana kufanya chumba kuwa na hewa safi na laini zaidi muda wote na hilo linakuwa ni muhimu zaidi kadiri chumba husika kinavyotumiwa na watu wengi zaidi.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *