USIMAMIZI WA MRADI WA UJENZI UFANYIKE KWA ORODHA NA NAMBA.

Usimamizi wa mradi wa ujenzi ni eneo lenye udhaifu mkubwa katika tasnia nzima ya ujenzi kwa ujumla, sehemu kubwa ya miradi ya ujenzi hujikuta kwenye changamoto kwa sababu ya udhaifu katika usimamizi wa ujenzi ambao unatokana na sababu mbalimbali. Udhaifu katika usimamizi wa mradi wa ujenzi ndio hupelekea makosa mengi ya kiufundi, mradi kushindwa kumalizika ndani ya muda uliopangwa, ubora wa kazi, mivutano na mamlaka mbalimbali za ujenzi n.k. Changamoto za eneo la usimamizi wa miradi wa ujenzi zimekuwepo miaka mingi na wakati mwingine hufikiriwa kwamba labda ni ufinyu wa bajeti kwenye eneo la ushauri wa kitaalamu, kitu ambacho kina ukweli kwa kiasi lakini sio kwa asilimia mia moja kwani hata miradi ambayo eneo la ushauri wa kitaalamu linapewa bajeti ya kutosha bado changamoto huwepo japo zinaweza kupungua kiasi.

USIMAMIZI WA MRADI WA UJENZI KWA ORODHA

Ili kukabiliana na changamoto na udhaifu wa kwenye mradi wa ujenzi kinachotakiwa kufanyika ni kuendesha usimamizi wa mradi kwa kutumia orodha na namba. Kwamba kwa kila hatua ya ujenzi kuwe na orodha ya kazi zinazotakiwa kufanyika, namna zinavyotakiwa kufanyika, kwa viwango vinavyotakiwa kufikiwa pamoja na matokeo yanayotarajiwa kuonekana. Orodha ya namna hii inatakiwa kutumika kwenye kila hatua ya ujenzi kuanzia kwenye kutengeneza michoro ya ramani mpaka kukamilisha jengo lenyewe ambapo orodha hizi zitatakiwa kuandaliwa na msimamizi mkuu wa mradi wa ujenzi kwa ushirikiano wa karibu kabisa na watalaamu wote pamoja na wadau wote wanaohusika kwenye mradi husika kila mmoja katika eneo lake. Katika kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa msimamizi mkuu wa mradi wa ujenzi anatakiwa kuhakikisha kwamba watu wote wanaohusika kwenye mradi huu wanapewa namba maalumu za kuzifikia kwa kipindi fulani aidha kwa siku au wiki katika kazi wanazofanya. Kwa mfano mtu anayejenga tofali anaweza kupewa idadi ya tofaliamabzo anatakiwa kuzijenga kwa siku au mtu anayepiga jengo rangi kupewa kiasi cha mita za mraba anazotakiwa kuwa amekamilisha kwa siku. Namba hizi ndizo zitawasukuma watu kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha mradi husika unamalizika ndani ya muda uliopangwa kwa mahesabu ya kiasi cha kazi kitakavyofanyika kwenye kila kitengo baada ya kuongezea na muda kidogo wa dharura.

KUTUMIA ORODHA NA NAMBA KUTAPUNGUZA CHANGAMOTO KWA KIASI KIKUBWA

Aina hii ya usimamizi ikifanyika kwa umakini, usahihi na nidhamu ya hali ya juu inapunguza kwa kiasi kikubwa kabisa changamoto za usimamizi wa miradi ya ujenzi ambazo zimekuwa ni tatizo la muda sugu.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

1 reply
  1. Nicefory mgaya
    Nicefory mgaya says:

    Wafanyakazi wanatakiwa kulipwa kwa kutumia namba.Wasilipwe kwa siku wala kwa mwezi.Akitimiza namba zake mkaguzi anakuja kukagua kama amefanya vizuri analipwa kwa idadi ya namba alizotimiza.

    Reply

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *