RANGI ZA NYUMBA, NAMNA UNAWEZA KUZITUMIA KUENDANA NA MAANA ZAKE AU ISHARA ZAKE.

Watu wengi kwenye eneo la rangi hubaki njia panda, wakati wengine wanatamani kujua mpangilio sahihi wa rangi ili kuleta muonekano unaovutia wengine hutamani kujua maana za rangi ili kupangilia kufuatana na maana zake. Kimsingi rangi zimegawanyika katika makundi makuu mawili ambayo ni rangi zinawaka sana kama vile nyekundu, njano na rangi ya chungwa na rangi zilizotulia kama vile kijani, blue na zambarau. Hizi rangi zinazowaka sana zinaashiria uchangamfu, mabadiliko, kujichanganya na watu na kuteka umakini wa watu kuliko zile rangi zilizotulia wakati rangi zilizotulia zinaashiria utulivu, kutojichanganya na watu na kujiweka mbali na usumbufu mwingi wa watu.

TAFSIRI ZA RANGI KATIKA MAJENGO ZINAHITAJI KUTAFAKARI KWA KINA SANA NA ZINAENDANA PIA NA MAMBO YA KIIMANI KWA KIASI

Rangi nyekundu inaashiria kujibu au jambo kubwa linalohusisha hisia kutokea kutokana na jambo la kuibua hisia lililofanyika, rangi nyekundu inaweza kuleta msisimko na furaha, rangi nyekundu inaongeza hamu ya vitu, kuimarisha misuli, mapigo ya moyo na msukumo wa damu. Rangi nyekundu ndio rangi ambayo inaonekana kwa haraka kuliko rangi nyingine yoyote na inapelekea mtu aidha kuchukua hatua au kujibu mapigo. Rangi nyekundu huchochea machachari ya vitu, shauku, nguvu na kusisimua na kufurahisha ambapo ni rangi ya mapenzi, hatari, hasira na msisimko. Rangi ya chungwa inachochea kujichanganya na watu na kuleta kuridhika na kusaidia uwiano wa kiakili na afya ya akili, rangi ya chungwa imekaa kirafiki, inaleta uchangamfu na imekaa kimichezo. Rangi ya chungwa inaleta ubunifu, busara, furaha na urafiki. Rangi ya njano ni rangi ambayo iko kwa ajili ya kujiandaa kuchukua hatua mara moja ambapo inachochea mtu kuhisi njaa na hivyo kuhitaji kula kama unavyoona matunda mengi yakiiva yanakuwa ya njano na hata baadhi ya migahawa ambayo inafuata kanuni hizi za rangi huwa inapakwa sana rangi za njano. Rangi ya njano ni ya kung’aa na ni rangi ya furaha, matumaini, inayoleta mwangaza kiufahamu na uelewa kiakili.

RANGI ZINA MADHARA KISAIKOLOJIA KWA WATU NA MARA NYINGI HUTUMIKA KWA MAKUSUDI FULANI NA SIO SUALA LA UREMBO NA UMARIDADI PEKE YAKE.

Rangi ya kijani inaashiria utulivu na usalama ambapo inaleta uupya, amani ya ndani ya moyo na utulivu. Huwa tunaiona rangi ya kijana kama inayotangaza hali ya amani, ujana, maelewano na pumziko. Kijani ni rangi ya asili inayoleta uwiano na uzazi. Rangi ya bluu ni rangi yenye kutegemewa na inayoleta faraja ambayo hutumika sana katika biashara za aina mbalimbali. Tunaiona rangi ya bluu kama yenye kuleta faraja na utulivu, inayohamasisha, inayoaminika na kuleta ubunifu wa kimabadiliko ambapo wakati mwingine inaashiria huzuni na unyong’onyevu. Bluu ni rangi ya uupya, uhuru, ukweli na uaminifu na mamlaka. Rangi ya zambarau ni rangi inayoleta utata na ufahari, yenye gharama kubwa na ni rangi ya kifalme. Rangi ya zambarau ni rangi ya kiroho, inayoashiria utu, miujiza na ni rangi adhimu. Zambarau ni rangi ya tafakuri, mafumbo, akili ya ubunifu na uadilifu.

RANGI KATIKA UJENZI ZIKITUMIKA KWA USAHIHI ZINAWEZA KUATHIRI HATA MATENDO YETU NA MITAZAMO YOTE KWA MAZINGIRA HUSIKA

Rangi nyeupe tunaiona kama rangi halisi, yenye usafi, yenye utulivu na iliyopevuka na yenye mwanga. Ni rangi amani, matendo mema na yenye uchache. Rangi nyeupe inachanganywa na rangi nyingine kuzifanya zing’ae na kuleta ladha ya utamu zaidi. Rangi nyeusi inaleta hali ya kuhimiza, kujiamini, uimara, “u-serious”, uwepo na umashuhuri. Rangi nyeusi inaashiria giza, mashaka, ukisasa na kuleta kujiamini. Ni rangi inayoweza kuhusisha udanganyifu, ufahari wa ubora na uelewa mpana wa mambo. Rangi nyeusi inachanganywa na rangi nyingine kuzifanya ziwe giza zaidi, zilete mwonekano unaoashiria ujasiri zaidi na undani na ustarehe na werevu.

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *