USANIFU MAJENGO KATIKA NYAKATI ZA MISRI YA KALE (ANCIENT EGYPTIAN ARCHITECTURE)

Usanifu majengo wa nyakati za Misri ya kale haukuwa katika katika ufanano mmoja bali ni mfululizo wa ubunifu tofauti ambao ulikuwa na ufanano mkubwa katika nyakati tofauti katika kipindi cha zaidi ya miaka 2,500. Mfano mkubwa na maarufu wa usanifu majengo wa nyakati za Misri ya kale ni ujenzi wa mapiramidi makubwa hasa yale mapiramidi yaliyopo Giza. Lakini pia kulikuwa na ujenzi wa mahekalu makubwa, majumba ya kifalme, makaburi hasa makaburi ya mafarao na ngome kubwa na imara. Kwa sehemu kubwa malighafi zilizotumika katika ujenzi wa majengo makubwa katika Misri ya kale ni mawe na matofali ya kuchoma.

MAPIRAMIDI MAKUBWA MATATU YALIYOPO GIZA, MISRI YALIYOJENGWA KWA AJILI YA FARAO KHUFU, FARAO KHAFRE NA FARAO MENKAORE MIAKA 4,700 ILIYOPITA, YENYE UREFU WA MITA 138, SAWA NA JENGO REFU LA WASTANI WA GHOROFA 45.

Imani za kidini na imani za maisha baada ya kifo ndizo zilichangia ujenzi wa baadhi ya majengo wa mfano mapiramidi ambayo yalijengwa kwa ufanisi wa hali ya juu, uimara na teknolojia bora sana ya zama hizo kama makaburi ya mafarao ambayo yalikuwa na umuhimu mkubwa kidini kisiasa na uhakika wa maisha bora na sahihi baada ya kifo. Masanamu makubwa kama ile sanamu kubwa ya “Sphinx” iliyojengwa kwa ajili ya Farao Khafre pia ilikuwa na umuhimu mkubwa sana kiimani. Baadhi ya sanamu zilipangwa rangi nzuri sana na nyingine zilipakwa rangi ya dhahabu huku dhahabu nyingine nyingi sana zikiwekwa sambamba na maeneo ya kumbukumbu na sana za watu mashuhuri.

USANIFU MAJENGO WA MISRI YA KALE, SANAMU KUBWA SANA MAARUFU KAMA “SPHINX” ILIYOPO GIZA, MISRI YA FARAO KHAFRE ILIYOJENGWA MIAKA 4,700 ILIYOPITA

Kutokana na uhaba wa miti na mbao katika Misri ya kale sehemu kubwa ya ujenzi ilitumika zaidi mawe na matofali ya kuchoma pamoja na aina nyingine za malighafi zilizopatikana ardhini na kwenye udongo. Mapambo mbalimbali kwenye mahekalu ya Misri ya kale na majumba makubwa kama vile baraza ya kipekee katika la kuingilia hekaluni na milingoti mingine mirefu zaidi mbele yake pamoja na mnara mkubwa kwa mbele maarufu kama “obelisk” yaliweza kuleta utambulisho wa tofauti wa usanifu majengo wa Misri ya kale ambao uliendelea kuigwa na tamaduni nyingine za kale kama Wayunani, Warumi na hata mpaka sasa maeneo mengine duniani na hasa Ulaya.

HEKALU KUBWA LA ISIS LILILOPO PHILAE, MISRI LILILOJENGWA MIAKA 2,380 ILIYOPITA KATIKA MISRI YA KALE

Mahekalu makubwa ya Misri ya kale kama hekalu la Karnak lililopo Luxor, Misri na hekalu la Isis lililopo Philae, Misri pamoja na mahekalu mengine mengi ya Misiri ya kale yenye urefu kwenda juu wa kufikia mita 120 au zaidi yamekuwa alama muhimu na maarufu ya Usanifu majengo duniani yakipewa hadhi ya Urithi wa dunia na Umoja wa mataifa tangu miaka ya 1970’s.

HEKALU KUBWA LA KARNAK LILILOPO LUXOR, MISRI LILILOJENGWA KATI YA MIAKA 4,000 NA 3,800 ILIYOPITA

Aina nyingine za mapambo kama vile urembo wa kwenye kingo za juu za paa bapa au vipengele vingine vya kwenye majengo, mipango miji ya miji ya kale, mipangilio ya bustani za kwenye makazi, miji na majumba ya kifalme yamekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya fani ya usanifu majengo tangu tamaduni na ustaaarabu wa Misri ya kale.

HOTEL KUBWA YA KIFAHARI YA LUXOR ILIYOPO LAS VEGAS, MAREKANI AMBAYO IMEJARIBU KUIGA STAILI YA USANIFU MAJENGO YA MISRI YA KALE

Licha ya muendelezo wa baadhi ya vipengele katika tasnia ya usanifu wa mjengo kutokea Misri ya kale kuchanganyika na mwendelezo kutoka tamaduni nyingine mbalimbali kuendelea kukua na kuja na ubunifu bora zaidi ambao umechangia tasnia nzima ya usanifu majengo mpaka zama za sasa lakini pia kuna maeneo mengine urithi huu wa kutokea Misri ya kale umechukuliwa moja kwa moja na kutengeneza majengo ya kifahari sana dunia nzima.

HOTEL KUBWA YA KIFAHARI YA LUXOR ILIYOPO LAS VEGAS, MAREKANI ILIYOJARIBU KUIGA STAILI ZA USANIFU MAJENGO ZA MISRI YA KALE

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *