USANIFU MAJENGO WA NYAKATI ZA UYUNANI YA KALE(ANCIENT GREEK ARCHITECTURE).

Usanifu wa majengo wa nyakati za Uyunani ya kale na baadaye Rumi ya kale ni kati ya staili ambazo zimekuwa na ushawishi mkubwa sana kihistoria kwa namna ambavyo majengo mengi yamekuwa yakijengwa kwa karne nyingi zilizopita n ahata mpaka sasa. Usanifu majengo wa Uyunani ya kale ulikuwa na ushawishi mkubwa kiasi kwamba kati ya maajabu saba ya dunia ya kale matano kati ya hayo yalikuwa ni majengo mbalimbali ya Uyunani ya kale. Kati ya hayo kulikuwa na mahekalu makubwa, masanamu makubwa, makaburi, majengo makubwa ya kijamii n.k. Hata hivyo usanifu majengo ya Uyunani ya kale ilipata umaarufu mkubwa sana kupitia mahekalu yake makubwa sana na mengi sana ya aina tofauti tofauti ambayo mengi kati ya hayo yaliweza kuigwa na kuendelezwa katika Rumi ya kale. Eneo lingine ambalo limeleta umaarufu sana katika usanifu wa majengo katika Uyunani ya kale ambalo limejitofautisha sana ni ujenzi kumbi kubwa za kijamii(theatres) ambazo pia zilijengwa kwa stili mbalimbali za tofauti.

HEKALU LA ATEMISI AU “HEKALU LA DIANA” LA UYUNANI YA KALE AMBALO LIMEKUWA NI ALAMA MUHIMU (ICON) YA USANIFU MAJENGO WA STAILI YA UYUNANI YA KALE

Katika usanifu majengo wa Uyunani ya kale zilitengenezwa kanuni maalum za mipangilio mitatu ya namna ya usanifu majengo na ujenzi unapaswa kufanyika zilizopewa majina ya mpangilio aina ya Doric, mpangilio wa aina ya Ayoni na mpangilio wa aina ya Korintho. Mpangilo wa aina ya Doric ambao ulikuwa maarufu zaidi na ulitumika maeneo mengi zaidi ulikuwa mpangilio rahisi na wenye mistari ilinyooka isiyo na mambo mengi. Mpangilio wa aina ya Ayoni ulikuwa na na mistari mingi iliyobanana zaidi, urembo kwa juu ya nguzo au vipengele vingine pamoja na urembo wa maduara kwa pembeni, staili hii nayo ilitumika kwa kiasi katika Uyunani.

KANUNI YA MIFUMO YA MIPANGILO MITATU MUHIMU YA UYUNANI AMBAZO ZIMEKUWA UTAMBULISHO WA STAILI ZA USANIFU MAJENGO ZA UYUNANI YA KALE.

Mpangilio wa tatu aina ya Korintho ulikuwa ni mpangilio wenye urembo mwingi sana, wenye vitu vingi sana uliokuwa unachukua sehemu kubwa ya shingo ya jengo au kipengele cha jengo, mpangilio huu wa aina ya Korintho haukupata umaarufu mkubwa sana katika Uyunani ya mwanzoni lakini baadaye katika maeneo ambayo tamaduni za kiyunani zilisambaa(Hellenistic culture) ulipata umaarufu zaidi na baadaye ulikuja kuigwa na kutumika sana katika Rumi ya kale. Mipangilio hii aina tatu iliyotumika sana katika Uyunani ya kale ilipata umaarufu kwa ujumla kwani ilikuja kuwa kama kanuni ya mwongozo katika Usanifu majengo katika Uyunani ya kale na kwa kiasi kikubwa ikaja kuigwa na kwenye Rumi ya kale pia.

JENGO LA HEKALU LA UYUNANI YA KALE LIKIONYESHA UHUSIANO KATI YA NGUZO NA KITAKO CHA JENGO, IKIWA NI STAILI YA USANIFU ILIYOKUWA MAARUFU KATIKA UYUNANI

Katika mahekalu ya Uyunani ya kale kulianzishwa pia utamaduni maalum wa kutengeneza eneo/chumba kitakatifu ambacho kiliwekwa pia na sanamu muhimu katika imani husika, utamaduni ambao kwa sehemu kubwa ulikuja kuigwa na mahekalu ya kwenye Rumi ya kale na baadaye makanisa ya kikristo baada ya ukristo kufanywa dini rasmi ya Warumi na kusambazwa duniani.

JENGO LA BUNGE LA MAREKANI LILILOPO WASHINGTON D.C., MAREKANI NI MFANO WA STAILI ZA USANIFU MAJENGO ZILIZOENDELEZWA KUTOKA UYUNANI YA KALE.

Usanifu majengo wa Uyunani ya kale pia ulianzishwa utamaduni wa kutumia mawe ya aina mabo kama malighafi maalumu ya urembo urembo kwa maeneo maalum hasa ndani ya majengo, utamaduni huu wa kutumia mabo ulikuja kuendelezwa katika Rumi ya kale katika mahekalu na baadaye makanisa na hata majumba ya kifahari na mpaka leo hii bado imekuwa sehemu muhimu ya urembo wa ndani ya majengo inayoongeza hadhi ya jengo husika.

JENGO LA MAHAKAMA KUU YA MAREKANI LILILOPO WASHINGTON D.C., MAREKANI NI MFANO WA STAILI ZA USANIFU MAJENGO ZILIZOENDELEZWA KUTOKA UYUNANI YA KALE.

Usanifu wa majengo wa staili za Uyunani ya kale zimeanza kuigwa na kutumika maeneo mbalimbali duniani tangu miaka ya zamani za kale Wayunani walipoipiga na kuitawala Asia na kuanza kuingiza staili hizi kuanzia kwenye mahekalu ya Budha. Staili za usanifu majengo na ujenzi za Uyunani ya kale ziliigwa na kutumika kwa kiasi kikubwa sana katika Rumi ya kale ambazo pia ziliendelezwa sana katika Ulaya na maeneo mengine ya dunia ambayo yalikuwa chini ya mamlaka au ushawishi kutoka Ulaya.

JENGO LA BUNGE LA MAREKANI LILILOPO WASHINGTON D.C., MAREKANI LIKIWA NA MCHANGANYIKO WA STAILI ZA USANIFU MAJENGO ZINAZOJUMUISHA STAILI ZA KUTOKA UYUNANI YA KALE.

Tamaduni hizi za staili za usanifu majengo kutoka Uyunani kuanzia miaka 3,200 iliyopita na kuja kuendelezwa kuanzia tena miaka 2,500 iliyopita na baadaye katika Rumi ya kale zilikuja kufufuliwa na kupata tena umaarufu katika karne ya 18 na 19 huko Ulaya, hasa Ulaya magharibi ambapo watu walivutiwa sana na kuanza mpango maalumu wa kuzifufua.

JENGO LA KUMBUKUMBU YA RAIS WA 16 WA MAREKANI ABRAHAM LINCOLN MAARUFU KAMA “LINCOLN MEMORIAL” LILILOPO WASHINGTON D.C., MAREKANI NI MFANO MWINGINE WA STAILI YA USANIFU MAJENGO KUTOKA UYUNANI YA KALE.

Licha ya kwamba hata mpaka leo bado majengo mengi ni mchanganyiko wa staili mbalimbali katika historia ambapo kwa sehemu kubwa zinatokea Uyunani lakini pia kuna baadhi ya majengo kama sehemu ya kuenzi staili za usanifu za Uyunani ya kale yamejengwa moja kwa moja kwa staili ya Uyunani ya kale.

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790

1 reply
  1. UWEKEZAJI MAJENGO
    UWEKEZAJI MAJENGO says:

    Nimekuelewa sana kuhusu usanifu wa majengo kwenye historia ya kale.

    Umetumia lugha rahisi sana kufikisha ujumbe. Asante sana.

    Je zipo sanifu za kale ambazo zina umaarufu mkubwa mpaka nyakati za sasa?.

    Kama zipo ni zipi hizo rafiki yangu Sebastian Moshi?.

    Rafiki yako,

    Aliko Musa.

    Reply

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *