MUDA WA ZEGE KUMWAGILIWA MAJI(CURING) KATIKA JENGO NI ANGALAU SIKU 21.

Katika ujenzi hususan wa majengo, mifumo yote inayohusika na mihimili ya jengo hutumia zege ikiwa jengo husika halijatumia mihimili ya chuma. Hata hivyo majengo yanayojengwa kwa chuma ni machache sana ukilinganisha na majengo yanayojengwa kwa zege. Hivyo majengo mengi katika mifumo yake ya mihimili yaani nguzo(columns), maboriti(beams), zege ya sakafu(slabs) na ngazi hujengwa kwa kutumia kutumia zege ambayo ni mchanganyiko wa mchanga, kokoto na saruji. Uimara wa mihimili ya chuma huamuliwa kabisa tangu kiwandani na ipokuja kwenye eneo la ujenzi ni kazi ya kuifunga kwa usahihi lakini uimara wa mihimili ya zege hutegemea mchakato wake wa ujenzi unavyofanyika katika eneo la ujenzi.

NI MUHIMU KUZINGATIA MUDA WA UMWAGILIAJI KWA SABABU UNAAMUA UIMARA WA MIHIMILI YA JENGO KWA KIASI KIKUBWA

Moja kati ya vitu vinavyoamua uimara wa mifumo ya mihimili ya jengo ukiachana na mchanganyiko sahihi wa mchanga, kokoto na saruji ni umwagiliaji wa maji katika mifumo hiyo ya mihimili mara baada ya kumiminwa kitaalamu. Lengo la kumwagilia maji mara baada ya zege hilo kumiminwa ni ili kuruhusu zege husika kushikana vizuri likiwa bado bichi ili liwe na uimara wa kutosha kiasi cha kushindwa kuvunjika kiurahisi au kumomonyoka kiurahisi. Kwa kawaida zege hili linatakiwa kumwagiliwa maji mengi ya kutosha kila siku asubuhi na jioni kwa angalau siku 21 mfululizo ndipo linakuwa limekamata uimara wa kutosha kuendelea kukauka na kuwa na ubora unaotakiwa. Lakini hata hivyo licha ya kwamba zege hili linahitaji kumwagiliwa mfululizo kwa siku 21 lakini ikiwa kuna ujenzi unatakiwa kuendelea juu yake baada ya kumiminwa, ujenzi huu unaweza kuendelea hata baada ya siku 7 peke yake baada ya kumiminwa. Hivyo ujenzi unaweza kuendelea baada ya siku 7 huku umwagiliaji wa maji(curing) ukiendelea mpaka siku 21 bila kuathiri kazi ya ujenzi.

UMWAGILIAJI (CURING) UFANYIKA KILA SIKU ASUBUHI NA JIONI BILA KUKOSA

Suala la umwagiliaji wa mifumo ya mihimili katika jengo (curing) maarufu kama zege ni jambo ambalo mara nyingi limekuwa likizembewa kwa kutomwagilia kwa usahihi au kwa muda unaopangwa kutokana na kwamba mara nyingi kazi katika eneo la ujenzi husimama kwa muda na hivyo kukosekana umakini kitu ambacho hupelekea mfumo wa mhimili kukosa uimara wa kutosha. Ni muhimu sana kuweka umakini mkubwa katika hatua hii ya umwagiliaji (curing) katika kuhakikisha ubora sahihi wa mifumo ya mihimili ya jengo.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

1 reply

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *