KWA NINI BAADHI YA WATU WANAPENDA KUJENGA KWA TOFALI ZA KUCHOMA?

Wapo watu wengi ambao wanapofikiria kuhusu malighafi za ujenzi kwenye suala la tofali huwa akili zinawapeleka kwenye tofali za kuchoma ambazo kwa vyovyote ndizo wanategemea kujengea nyumba zao. Unaweza kujiuliza ni kwa nini baadhi ya watu wanapenda zaidi tofali za udongo za kuchoma badala ya tofali zinatengenezwa kwa mchanga na saruji. Labda tuangalie sababu kadhaa.

Sababu kuu ya kwanza ya watu kutaka kutumia zaidi tofali za kuchoma ni upatikanaji katika eneo husika. Kuna baadhi ya maeneo au mikoa kama vile mikoa ya nyanda za juu kusini Tanzania na baadhi ya maeneo mengine ambayo tofali za kuchoma zinapatikana kiurahisi na kwa wingi kuliko tofali za mchanga na saruji na hivyo inakuwa ndio mbadala pekee wa uhakika unaotegemewa na watu.

Lakini kuna maeneo kama vile maeneo ya pwani ambapo mchanga unapatikana kwa wingi na tofali za kuchoma hazipatikani kwa wingi lakini bado kuna watu wanapenda kutumia tofali za kuchoma na hapa sababu ya pili inakuja kwamba ni mapenzi pia, kuna watu huwa wanazipenda sana tofali hizi za kuchoma na inapofika wakati wa kujenga wanazitafuta popote kwa gharama yoyote kwa ajili ya miradi yao.

WATU HUPENDELEA KUJENGA KWA TOFALI ZA KUCHOMA KAMA SEHEMU YA UREMBO YA JENGO LENYEWE

Sababu nyingine ya tatu ni watu kuamini kwamba tofali za kuchoma ni imara, hii ni imani ambayo watu wengi wanayo ambayo ina ukweli fulani lakini unaohitaji ufafanuzi zaidi, kwamba tofali za kuchoma ni imara sana ukilinganisha na tofali za mchanga na zinadumu kwa miaka mingi sana na majengo yanayojengwa kwa tofali hizi huwa imara sana.

Watu wengine hupenda kutumia tofali za kuchoma kwa sababu ya umaridadi na urembo zilizonazo ambapo mara nyingi watu huchagua nzuri zilitengenezwa kwa usahihi na kunyooka kwa makini kabisa na kuzitumia kujenga kisha kutofanya finishing ya “plastering” wala rangi na badala yake rangi ya tofali yenyewe kama ilivyo au kwa kuongezewa na rangi kama “polish” ya kung’aa ndio inakuwa finishing yake.

Sababu nyingine ya tano ambayo baadhi ya watu hupendelea kutumia tofali za kuchoma badala ya zile za mchanga na saruji ni gharama. Watu huamini kwamba tofali hizi ni za bei rahisi na hivyo kuona kwamba wanapunguza gharama sana kwa kutumia aina hii, japo kwa sehemu ni kweli kwamba ni za gharama nafuu kidogo lakini kama zinasafarishwa umbali mrefu gharama yake kwa ujumla pia huongezeka sana.

TOFALI ZA KUCHOMA HUWEZA KUONGEZA UMARIDADI NDANI YA NYUMBA

Sababu nyingine ya sita ya watu kupenda kutumia zaidi tofali hizi za kuchoma ni pamoja na mazoea na ushawishi, unakuta mtu tangu akiwa mtoto amekuwa akiona tofali hizi zikitumika katika mazingira yake kila siku na kuzoea kwamba hizo ndizo tofali sahihi kwa ajili ya ujenzi, na hivyo anapofikiria kujenga anaamua kutumia hizo kwa sababu anaamini ndizo sahihi zaidi kwa ajili ya mradi wake. Lakini pia ushawishi kutoka kwa watu wa karibu na hasa mafundi ambao wana uzoefu wa kiufundi na tofali hizi huwa sababu pia ya watu kutumia tofali hizi kwenye ujenzi.

Wakati mwingine pia mafundi kwa sababu ya uzoefu katika kutumia tofali hizi kwa sababu pia aina nyingi huwa sio nzito katika kubebeka na hivyo kurahisisha kazi ya ujenzi kufanyika kwa haraka na pengine kwa makini zaidi huamua kutumia tofali hizi katika kujengea.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

1 reply

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *