ELEWANA NA VIONGOZI WA SERIKALI YA MTAA JUU YA KIWANJA CHAKO KABLA HUJAANZA KUJENGA.

Kama kuna mambo yanayoendelea ambayo huyajui kuhusu kiwanja chako utashangazwa jinsi yatakavyojitokeza mara utakapoamua kujenga. Baadhi ya viwanja huwa vinauzwa vikiwa na utata au kukiwa bado kuna changamoto ambazo hazijatatuliwa kuhusiana na viwanja hivyo.

Lakini huwa hakuna namna ya kutatua au wakati hata wahusika unakuta hawana taarifa yoyote ya kinachoendelea juu ya kiwanja husika mpaka pale mtu anapoamua kuanza kujenga ndio kila kitu huonekana wazi na wahusika kuanza kufuatilia na kueleza kila kitu kinachoendelea juu ya kiwanja husika.

Suala hili mara nyingi hutokea kwa ghafla bila mteja mwenyewe kujua na huwa ni suala linamshangaza kwa sababu hakuwa anajua hapo kabla kama kiwanja chake kiko kwenye mivutano, japo ambalo hupelekea kumkwamisha mambo yake na wakati mwingine hata kumwingiza hasara pale mambo yanayojitokeza yanapoingilia ratiba ambazo zinahusisha muda wa mradi kukamilika na mambo ya malipo ya fedha.

Hata hivyo mara nyingi suala la kiwanja kuwa kwenye changamoto ni ambalo huwa linajulikana aidha na majirani hasa kama wanaishi eneo hilo au zaidi serikali ya mtaa ya eneo husika. Lakini kutokana na uzito na ugumu ambao huwa unakuwepo kwenye migogoro hiyo ni vigumu watu kushughulika na kesi hiyo ikiwa pande zote hazijawa tayari kuzungumzia suala hilo.

Hivyo ikiwa mtu unahitaji kuendeleza eneo lako au kwa kujenga nyumba au kufanya shughuli nyingine yoyote ya maendeleo ni muhimu kwanza kabla hujaanza hata kutengeneza ramani achilia mbali kujenga uonane kwanza na uongozi wa serikali ya mtaa husika na kuwaeleza kwamba unataka kuanza mpango wa kuendeleza eneo hilo upate maoni yao juu ya eneo husika.

Viongozi wa serikali ya mtaa husika pia huwa wanafahamu mambo mengine mbalimbali kuhusiana na eneo hilo na tabia za mtaa husika na hivyo watakutahadharisha mapema juu ya mambo hayo. Viongozi wa mtaa husika pia ndio mara nyingi hutoa taarifa kwa mamlaka za juu zaidi juu ya mwenendo wa jambo lolote kuhusiana na chochote kinachofanyika na hivyo watakueleza kila kitu ambacho hutokea kuhusiana na kile unachokwenda kufanya.

Kwa maana hiyo suala la kuonana na viongozi wa serikali ya mtaa na kuwaeleza kile unachoenda kufanya katika eneo hilo ni suala muhimu sana na litakaloweza kukuepusha na usumbufu mwingi usiouhitaji pamoja na kukuokolea muda kwenye mambo ambayo pengine yangekukwamisha.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *