NI GHARAMA KUBWA IKIWA UJENZI UTAMALIZIKA BILA CHANGAMOTO.

Wote tunajua jinsi kila mtu huwa yuko makini sana na suala la gharama pale anapotaka kufahamu bei ya kitu chochote ikiwa anahitaji kweli kitu hicho. Hii ni hisia ya kisaikolojia kwa kila binadamu duniani ambayo imepandikizwa ndani yetu kutokana na uhaba wa upatikanaji wa rasilimali fedha au thamani nyingine mbadala ukilinganisha na umuhimu wake katika maisha yetu.

Kweli ni sahihi na muhimu sana kwa mtu yeyote kuweka umakini mkubwa kwenye kuhakikisha kwamba thamani ya huduma au bidhaa anayopata inalingana na kiasi cha fedha anachotoa kwa sababu tofauti na hapo anakuwa ameibiwa na hakuna mtu anapenda kuibiwa, na hata katika uchumi kwa ujumla ni makosa pale ambapo mtu anapolipia fedha nyingi zaidi ya thamani anayopata.

Lakini pamoja na kwamba tunapaswa kuweka umakini mkubwa kwenye kuhakikisha kwamba gharama za huduma za ujenzi tunazolipia zinaendana na thamani inayotolewa bado hiyo haimaanishi tusiangalie pia kwa upande wa huduma husika na kulipia vile inavyostahili na kuweka uwiano mzuri katika eneo hili. Watu wengi wamekuwa wakishindwa kuangalia uwiano huu na badala yake kukazana kupunguza gharama peke yake bila kujali ubora wa huduma wanayopata na kujikuta kwenye changamoto kubwa.

Kuna dhana maarufu inayofahamika inayosema kwamba huwezi kuiibia asili, asili ndio ambayo inahakikisha kwamba kunakuwa na uwiano sahihi kwenye kila kitu duniani. Yaani kila kitu kinalipwa kwa kadiri ya vile kinavyostahili na unapojaribu kuingiza ujanja sio rahisi ukapata kile haswa unachotaka, yaani kila kitu kwa kadiri ya ubora wake kinahitaji kulipwa thamani inayokistahili.

Uhalisia huu wa asili umekuwa unawagharimu wengi wanaojaribu kutaka kuiibia asili ambao wanatengeneza mazingira ya kuhakikisha wanapata kitu kwa gharama ndogo kabisa lakini chenye ubora mkubwa. Kwa mfano mtu anaweza kusema yeye ana mafundi ambao atawalipa yeye moja kwa moja ambapo anajua atawalipa kidogo sana kisha anahitaji wewe uwasimamie kwa usahihi wasiharibu kazi ambapo anajua atakulipa kiasi ambacho mtakubaliana kwa utaratibu huo ambao kwake itakuwa ni gharama nafuu kuliko kukupa mkataba wa jumla moja kwa moja.

Akiangalia ataona kwamba ameokoa gharama kiasi fulani kwa kufanya hivyo lakini changamoto zinajitokeza tena kivingine. Kwanza atakutana na usumbufu wa namna ya kuendesha kazi hiyo kwa sababu mara nyingi atashindwa kupangilia namna kazi inavyofanyika na utaratibu wa ulipaji wa fedha unaoendana nao lakini pia msimamizi akiwa hayuko katika maelewano na wanaosimamiwa na hawajuani uwezo wala mfumo wa ufanyaji kazi, kunaweza kuleta migogoro na kutoelewana na hata tafsiri ya ubora wa kazi ikawa tofauti na viwango tofauti.

Lakini pia nguvu ya kuwawajibisha wahusika kwa kazi iliyofanyika vibaya au kimakosa haitakuwepo kwa msimamizi na badala yake itakuwepo kwa mteja, kitu ambacho kitapelekea msimamizi kushindwa kushinikiza mabadiliko kwa kiwango kinachostahili. Kwa maana hiyo ubora wa kazi ni wa mashaka sana na uwezekano wa kazi kuharibika au kuchelewa ni mkubwa sana pia. Kwa kifupi msimamizi hatakuwa msimamizi bali atakuwa ni mtazamaji zaidi ambaye yuko kwa ajili ya kukosoa kazi.

Kazi inapoharibika sasa unakuja kugundua kwamba urahisi huo wa gharama unakuja unakuja na gharama kubwa na pengine unaweza kujikuta kwenye hasara kubwa kiasi kwamba ile gharama ndogo ya kumpa msimamizi mkataba wa kazi yote ni gharama nafuu sana ukiangalia uharibifu uliotokea.

Karibu sana

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *