KWENYE MRADI WA UJENZI USIWEKE MTAZAMAJI MKOSOAJI WEKA MSIMAMIZI.

Moja kati ya maeneo ambayo yamekuwa yakifanyika makosa makubwa kwenye usimamizi wa miradi ya ujenzi ni namna ambayo msimamizi anahusiana na mtekelezaji au wajenzi katika mradi. Wateja wengi wamekuwa wakifanya maamuzi ya kuweka kuingia mkataba na fundi au mkandarasi kisha kuweka msimamizi ambaye atakuwa anahakikisha kazi inafanyika kwa usahihi na kwa viwango vinavyokubalika kwa kuzingatia makubaliano yote yaliyofikiwa.

Changamoto ambayo imekuwa inajitokeza ni kwamba licha ya msimamizi huyu kuweza kufuatilia na kuonyesha makosa mbalimbali ambayo hufanyika katika mradi wa ujenzi lakini hana uwezo wa kuzuia makosa hayo yasifanyike bali ana uwezo wa kuyaona na kuyakosoa ili yarekebishwa baada ya kuwa yameshafanyika kwa sababu yeye sio mtekelezaji wala hapangi namna kazi inafanyika bali anakagua na kuonyesha maeneo ambayo makosa yamefanyika au yanafanyika.

Hii ni kwa sababu pia msimamizi sio anayechagua mafundi wa kufanya utekelezaji wala sio anayewaelekeza ni nini cha kufanya katika kazi hiyo bali kazi yake ni kukagua kilichofanyika na kuonyesha kwenye makosa kisha kutoa mapendekezo. Lakini ubora wa kazi kwanza unaanza na uchaguzi sahihi wa mafundi na kisha usimamizi sahihi, hivyo pale mtekelezaji anayefanya kazi hiyo na mafundi anapokuwa huru kufanya kazi yake msimamizi anabaki kama mtazamaji na mkosoaji.

Sasa ikiwa kazi ya kujenga amepewa mkandarasi mwingine na msimamizi wa kazi hiyo(chief consultancy) ni mwingine kinachotakiwa kufanyika ni kuweka mahusiano ya uwajibikaji kwa pande zote mbili. Kwanza msimamizi ambaye ndiye anahakikisha kazi inajengwa kwa viwango anatakiwa kupewa nguvu ya kimamlaka juu ya mkandarasi ambaye ni mtekelezaji kwa maana ya kwamba msimamizi ndiye atakayekubali na kupitisha kazi hiyo kama amaeiona kwa imefanyika kwa usahihi.

Msimamizi akipitisha kazi ndipo mtekelezaji, mjenzi au mkandarasi ataweza kuidhinishiwa malipo na kuruhusiwa kuendelea hatua za mbele zaidi za kazi hiyo. Hii itapelekea ushirikiano mkubwa zaidi wa kiufundi kati ya msimamizi na mtekelezaji ambapo mtekelezaji hatathubutu kufanya kitu kiholela au chini ya kiwango akijua kwamba kazi yake haitapitishwa na msimamizi na yeye kulipwa na kuendelea na kazi.

Msimamizi naye hapa atatakiwa kubeba lawama yeye sambamba na mtekelezaji huku yeye akibeba lawama zaidi na kuwajibika kwa uzembe wowote wa kitaalamu utakaokuwa umejitokeza. Hii itapelekea kuwepo kwa uwajibikaji mkubwa kwa pande zote mbili na uwezekano wa kazi kufanyika kwa ubora zaidi utakuwa ni mkubwa na mivutano kati ya pande zote mbili utakuwa ni wa kiwango kidogo kwa sababu wote watalazimika kuwa sehemu ya kupigania ubora badala ya kurushiana lawama.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *